BAVICHA waitaka serikali kujifunza kupitia Mapacha


Baraza la Vijana wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limeitaka serikali kujifunza kupitia kifo cha mapacha walioungana, Maria na Consolata ambao wamefariki Jumamosi Usiku wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa Iringa.


Kupitia tarifa ya salamu za rambi rambi iliyotolewa na Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrick Ole Sosopi, amesema kuwa kama taifa inabidi kukubaliana na ukweli kuwa sekta ya afya ina changamoto nyingi ikiwepo huduma za Afya na uduni wa mazingira hivyo viongozi wanapaswa kushughulikia matatizo hayo na siyo kuwa mbele katika kushiriki misiba.

Aidha Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema kwamba Taifa limepoteza nguvu kazi ambao walikuwa na malengo pamoja na ndoto kubwa katika taifa pindi watakapokuwa wamemaliza masomo yao.

Pamoja na hayo BAVICHA wametoa shukrani na pongezi kwa kanisa Katoliki kwa kuwalea mapacha hao ambao wanatambulika kama mashujaa kwa taifa katika kipindi chote cha uhai wao.

Maria na Consolata walizaliwa Novemba 19, 1997 na wamefariki  Juni 2, 2018 ambapo enzi za uhai wao walikataa kutenganishwa miili yao na waliishi kwa miaka 21 wakiwa wameunga hivyo hivyo.

Septemba mwaka jana, baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, Maria na Consolata walijiunga na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Iringa. Walianza kuugua maradhi ya moyo na Desemba mwaka jana, wakahamishiwa taasisi ya maradhi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili.

Leo hii Maria na Consolata watazikwa kwenye kaburi moja litakalokuwa na misalaba miwili katika makaburi ya viongozi wa dini yaliyopo Tosamaganga mkoani Iringa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad