Benki 10 matatani kwa kupitisha fedha zilizoibwa NYS
0
June 01, 2018
Gavana wa Benki Kuu, Dk Patrick Njoroge
Nairobi, Kenya. Wakati vigogo kadhaa wanashikiliwa kwa tuhuma za ufisadi, benki 10 za kibiashara zinazotuhumiwa kupitishia fedha za Mfuko wa Taifa wa Huduma ya Vijana Kenya (NYS), ziko matatani.
Hata hivyo, benki hizo zimeonyesha ukimya kuhusiana na ukwapuaji wa fedha hizo, licha ya Serikali kupitia kwa mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, George Kinoti kuzitaka kuwajibika.
Uchunguzi kuhusiana na fedha za NYS unaendelea chini ya Benki Kuu, Ofisi ya Mkurugezi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Huduma ya Taifa ya Upelelezi (NIS) na Mamlaka ya Mapato (KRA).
Tayari ofisi ya DCI na Benki Kuu zimeonya kuhusu madhara ambayo benki zilizotumika kuchepusha fedha hizo zinaweza kuyapata ikiwamo kufutiwa leseni za uendeshaji.
Gavana wa Benki Kuu, Dk Patrick Njoroge alisema hivi karibuni kuwa wizi wa fedha za NYS kupitia vocha za kughushi za malipo ulifanikishwa na mabenki ‘kwa makusudi’. “Ni kwa jinsi gani unaweza kufanya kosa katika mambo ambayo unayafahamu?” Alihoji Dk Njoroge.
Alhamisi, mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, George Kinoti pia alizionya benki kuacha kujificha nyuma ya uchunguzi unaoendelea. “Wanapaswa kutoka nje wakiwa wasafi kama mwongozo unavyosena na kusema iwapo taratibu zilikiukwa, lakini waambieni kwamba wamegusa namba mbaya. Sisi na CBK (Benki Kuu) tunawafuata,” alisema.
Licha onyo hilo, hakuna benki kati ya zilizotajwa iliyokuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kina isipokuwa Diamond Trust Bank ambayo ilisema inatimiza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na miongozo ya kibenki.
Benki ya Stanbic ilisema maofisa wake “wamefungwa na mahitaji ya kuhifadhi usiri na kwa hiyo taarifa yoyote (juu ya yale waliyofanya wakati pesa ilipoingia) yanaweza kujadiliwa na maofisa walioidhinishwa.”
Benki ya Biashara Kenya (KCB), ambayo pia inafuatiliwa ilikataa kutoa maoni juu ya masuala yoyote yanayochunguzwa ikiwa ni pamoja na yale waliyoyafanya wakati fedha za NYS zilipokwapuliwa.
“Kama unavyojua, suala hili liko chini ya uchunguzi katika mamlaka za uchunguzi na ni suala la kisheria. Kwa hiyo hatutaki kutoa maoni,” ilisema taarifa.
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Kenya, Lamin Manjang pia alikataa kutoa maelezo akisema, “hatuwezi kutoa maoni juu ya suala hilo kwa kuwa linafanyiwa uchunguzi na taasisi za Serikali zenye mamlaka.”
Vilevile, Benki ya Barclays Kenya ilisema haitaki kuathiri ubora wa mchakato wa uchunguzi ikisisitiza kuwa, “tunauchukulia kwa umakini na kwa hiyo tunashirikiana kikamilifu na taasisi za uchunguzi.”
“Tunajua uchunguzi unaoendelea katika NYS. Jambo hili linafuatiliwa na mamlaka za Serikali. Zaidi ya hayo hatuwezi kutoa maoni juu ya jambo hilo, bado ni jambo la uchunguzi.”
Gazeti la Daily Nation, lilipeleka barua za ombi la kupata maoni katika Benki ya Equity, Benki ya Ushirika na Benki Kuu ambazo pia zimetajwa na wachunguzi, lakini wahusika hawakujibu chochote.
Hata hivyo, licha ya onyo la gavana na mkurugenzi wa upelelezi, benki zinapaswa kuchukulia kwa tahadhari suala hilo ikizingatiwa kwamba hazitakiwi kuchunguza taarifa za wateja wao, kukamata au kuchukua fedha zao.
Vigogo washikiliwa
Vigogo watano ambao ni miongoni mwa watu 24 waliokamatwa kwa tuhuma za ufisadi wa fedha za NYS, wanashikiliwa mahabusu kutokana na amri ya mahakama.
Vigogo hao wenye nyadhifa za juu ni Lilian Omollo (katibu mkuu wa Wizara ya Vijana, Sammy Mbugua (mkaguzi mkuu katika Wizara ya Utumishi wa Umma), Micheal Ojiambo (mkurugenzi wa usimamizi katika wizara hiyo), Clement Murage (mhasibu mkuu wa zamani) na Richard Ndubai (mkurugenzi mkuu wa NYS).
Tags