Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesitisha mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma stashahada (diploma) kuanzia mwaka wa masomo 2018/2019 kama ilivyokuwa imetangaza Mei 10 mwaka huu.
HESLB ilitoa mwongozo unaosimamia utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 ambao ulieleza kuwa ingeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na kuwa utaratibu wa kuomba mikopo hiyo ungetolewa baadaye.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru inasema hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha kuwa kiasi chote cha Sh427.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2018/2019 kinaelekezwa kwa wanafunzi wenye mikopo hivi sasa na waombaji wapya wahitaji ambao wana sifa za kujiunga na kozi za shahada tu ambao ndiyo walengwa wakuu.
“Hivyo basi, tunatoa wito kwa wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na masomo ya shahada katika taasisi za elimu ya juu na ambao ni wahitaji wa mikopo kuhakikisha wanasoma kwa makini mwongozo wa utoaji mikopo na kuuzingatia,” inasema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017/2018, takribani maombi 10,027 ya mikopo yaliyowasilishwa Bodi ya Mikopo yalikuwa na upungufu kama vile kutosainiwa, kutokuwa na viambatanisho sahihi.