Biashara ya shirika la ndege la AIR Tanzania Company Limited (ATCL) imepanda thamani kwa kipindi cha miaka miwili licha ya kuwa na abiria wachache waliotumia ndege zake kusafiria
Mkurugenzi wa biashara wa ATCL Patrick Ndekana aliambia gazeti la Daily News kwamba biashara za shirika hilo la serikali iliongezeka kutoka asilimia 2.5 mwaka 2016 hadi asilimia 42.6 mwisho wa mwaka jana huku ikiwa na ndege mbili pekee zinazofanya kazi.
Amesema kuwa wana matumaini kwamba biashara hiyo itaimarika zaidi baada ya kununuliwa kwa ndege mpya.
''Mwaka huu biashara yetu itaongezeka hususan baada ya kuwasili kwa ndege ya tatu kubwa aina ya Bombadier Q-400s na baadaye kuwasili kwa Bombadier nyengine mbili za Cs 300s ambazo zitakuwa na viti vingi'', alisema.
Kwa sasa shirika hilo linamiliki ndege tatu aina ya Q-400 katika maeneo 10 tofauti nchini, mbali na kuelekea Comoro.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka jana, shirika hilo limekuwa likisafirisha abiria wachache na kufanya safari chache ikilinganishwa na washindani wao.
ATCL inapanga kuleta ndege hizo mpya kupitia kuongeza safari hususan katika maeneo ya Kaskazini , magharibi kaskazini mashariki.
Ndege hizo za serikali zinapanga kuanzisha safari za kuelekea Bujumbura, Burundi kupitia Kigoma na Entebbe, Uganda kupitia Kilimanjaro.