Chadema Wahoji Iwapo Serikali Tayari Imelipwa na Barrick Gold na Accacia


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kimehoji Bungeni Ijumaa iwapo serikali tayari imepokea malipo kutoka kwa kampuni za madini, Barrick Gold na Accacia.

Kampuni ya Barrick Gold

Wabunge wawili wa chama hicho cha upinzani Saed Kubenea (Ubungo) na Ryoba Chacha (Serengeti) walihoji kuhusu malipo hayo ya Dola milioni 300 yaliyokuwa yafanyike na kampuni ya Barrick Gold.

Kubenea alisema anashangaa kuona kitabu chote cha hotuba ya Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, hakina taarifa zozote kuhusu malipo hayo.

Kutokana na hali hiyo, alitaka maelezo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu hatua iliyofikiwa katika majadiliano baina ya timu ya serikali na Kampuni ya Barrick.

Kampuni ya Accacia

Wabunge wa Chadema pia walimtaka waziri huyo kueleza Dola bilioni 190 (Shilingi trilioni 424) zinazopaswa kulipwa na Acacia zitapatikana lini.

"Sisi tulitegemea Bunge letu tupewe taarifa ya kina kuhusu mazungumzo kati ya serikali na Acacia. Tuelezwe Shilingi trilioni 424 ambazo ni Dola bilioni 190 tungepata lakini bajeti nzima imekuja haijazungumzia makinikia," Kubenea alisema na kuongeza:

"Kwa kuwa mmoja wa wajumbe ni Waziri Kabudi, atuambie makinikia imefikia wapi mchanga uliozuiwa bandarini upo, utakuwapo hai lini, unasafarishwa, kiwanda cha kuchenjua kitajengwa lini?" Kubenea alisema.

Majibu ya Waziri Kabudi

Naye Waziri wa Katiba na Sheria Palamagamba Kabudi, ameliambia bunge kuwa mazungumzo kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold yanaendelea vizuri na yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni au katikati ya Julai 2018.

Amesema moja ya mambo ambayo yanayozingatiwa katika mazungumzo hayo kwa sasa ni namna ambavyo serikali italipwa na kampuni hiyo Dola 300,000 alizoziita za kishika uchumba.

Alisema "Inshallah fedha hizo zitalipwa" kwa kuwa mazungumzo baina ya pande zote mbili yanaendelea vizuri.

Profesa Kabudi pia aliweka wazi kuwa waliamua kuficha majina ya wajumbe wanaounda timu ya Tanzania katika majadiliano hayo kutokana na vitisho ambayo serikali ilikuwa ikipewa na baadhi ya Watanzania.

Kauli hizo za vitisho ni usemi uliokuwa ukitolewa kwamba haitaambulia chochote cha maana zaidi ya kuishia kushtakiwa kwenye mahakama za juu.

Kampuni ya TanzaniteOne

Katika ufafanuzi wake, Kabudi pia alizungumzia mikataba inayohusu madini ya tanzanite, akibainisha kuwa tayari serikali imelipwa na Kampuni ya TanzaniteOne.

“Ili kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania, serikali inafanya mazungumzo na kampuni nyingine za uchimbaji wa madini zikiwamo kampuni 10 zinazojihusisha na biashara ya madini ya tanzanite," alisema.

“Aidha, Kampuni ya TanzanieOne ambayo imeshaanza mazungumzo na serikali, imekubali kuilipa fidia serikali kutokana na ufanyaji wake wa biashara nchini na pia kampuni hiyo imekubali kulipa tozo na kodi zote inazotakiwa kulipa,” alieleza zaidi waziri huyo.

Hata hivyo, Profesa Kabudi hakutaja kiasi cha fedha kilicholipwa na Kampuni ya TanzaniteOne kwa serikali kutokana na kile alichosema watu wanaoidai serikali wataishtaki kutaka kulipwa madeni yao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad