CUF yawang'ang'ania Lipumba, Seif
0
June 08, 2018
NA FATUMA MUNA
Chama cha Wananchi CUF, kimeitaka Serikali kuunga mkono hoja ya Mbunge wa Jimbo la Chonga Mohamed Juma Khatib, kufanya ukaguzi lazimishi wa fedha za Umma ikiwa ni pamoja na Msajili wa vyama vya siasa Jaji Mutungi, Maalim Seif, Ibrahimu Lipumba wahojiwe walikopeleka Bilioni 2 za Chama.
Hayo yamesemwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma Mbarala Maharagande wakati akiwapongeza Wabunge wa chama hicho wakiongozwa na Mhe. Khatib, kwa kutekeleza wajibu wao vizuri na kuibua ufisadi wa fedha za umma unaofanywa watu aliowaita matapeli wa kisiasa, na wasaliti ndani ya CUF kwa njia ya Ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa nchini.
Katika kikao cha bunge Juni 5, 2018, wakati akichangia bajeti ya wizara ya Fedha kwa mwaka wa 2018/2019, Mhe. Khatib aliomba bunge lijadili na kupitisha azimio la Katibu Mkuu wa CUF-Chama cha Wananchi Mhe. Seif Sharif Hamad ahojiwe na vyombo husika ili aeleze ni kwa nini hakufunga na kuwasilisha taarifa ya mahesabu ya Chama kwa mwaka wa fedha wa serikali ulioishia Tarehe 30/6/2016 na kueleza ni wapi zilopo takriban Tshs. bilioni 2 zinazodaiwa kulipwa kwa CUF kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Katabazi Mutungi.
Mbarala amesema kwamba mbunge anapohoji juu ya matumizi mabaya ya fedha za serikali na kukubali mtu yeyote ambaye anaonekana kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma ahojiwe na kuchukuliwa hatua, Mbunge huyo anastahili kupongezwa na huo ndio utekelezaji wa jukumu la msingi la kuisimamia na kuishauri serikali.
Pamoja na hayo Mbarala amekanuasha taarifa za Seif kutowepo ofisini kwake kwa kusema kuwa "Katibu Mkuu yupo Ofisini kwake MaKao Makuu ya Chama cha CUF Mtendeni, Unguja Zanzibar akiendelea na Majukumu yake ya kila siku kama Kawaida. Kwa mujibu wa katiba ya CUF ibara ya 90 NA 93 Maalim Seif Sharif Hamad ndiye CHIEF ACCOUNTING OFFICER na wala si vinginevyo".
Hata hivyo Mbarala amesema Lipumba, Sakaya na Kambaya wanatakiwa kuwaomba radhi Watanzania kwa wizi wa Fedha za umma walioufanya hali ya kuwa si Viongozi halali wa CUF na kwamba Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililoketi Tarehe 28/8/2016 liliwasimamisha uanachama na baadae Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Tarehe 27/9/2016 kuwafukuza uanachana aidha, Mkutano Mkuu Maalum wa Tarehe 21/8/2016 uliridhia Maamuzi ya Lipumba kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa CUF toka mwaka 2015 Agosti 5.
Tags