Imeelezwa kuwa kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani ambapo inaelezwa kuwa ni makosa kwa gari la abiria kujaza mafuta sheli huku abiria wakiwa ndani, endapo akishtakiwa adhabu yake ni jela mwaka mmoja na faini isiyozidi laki tano.
Hayo yamebainishwa na Wakili Yohanes Konda katika mahojiano na eatv.tv ambapo amesema kuwa endapo dereva akibainika kufanya kosa hilo anaweza kutozwa faini isiyopungua Shilingi laki tatu ama kwenda jela mwaka mmoja.
“Sheria haijasema moja kwa moja ni kiasi gani lakini haitakiwi kuzidi laki tano, na endapo mtuhumiwa ni kosa lake la kwanza anaweza kupewa adhabu moja kati ya hizo lakini kama ni kosa la mara kwa mara hupewa vyote kwa pamoja”, amesema Konda.
Kumekuwa na mazoea ya madereva wengi wa daladala kujaza mafuta huku wakiwa na abiria, jambo ambalo mamlaka husika zimelipigia kelele lakini bila mafanikio.