DAR ES SALAAM:Ni zengwe zito! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wapenda ubuyu kuibua madai kuwa nyumba wanayokaa wazazi wa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Juma na ile ya baba yake Ally Salehe Kiba, Mzee Kiba hazina hadhi.
Watoa ubuyu hao walipiga simu chumba chetu cha habari na kuwataka wanahabari wetu wafanye uchunguzi wao kwa kulinganisha nyumba wanazoishi wazazi na zile wanazoishi mastaa hao.
“Unajua sisi vijana tukifanikiwa huwa tunawasahau wazee, Kiba na Diamond wanapaswa kujitathimini katika hili.
“Mimi napafahamu pale Magomeni anapokaa mzee Abdul, yaani ukiangalia nyumba yake imechoka sana.
“Tena ukifika pale utaona na mzee mwenyewe kama anabangaizabangaiza na vibiashara, mara auze viatu mara sijui auze mitumba, Diamond yeye yupo tu anapiga zake shoo za maana na kuishi kwenye mjengo wa maana kule Madale,” alisema mtoa ubuyu huyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Kessy, anayeishi jirani na baba Diamond, Magomeni-Kagera jijini Dar.
Mtoa ubuyu mwingine aliyeomba hifadhi ya jina lake, alizidi kumwaga ubuyu kuwa, kutokana na shughuli zake kufanyia Kariakoo, amekuwa akipita nyumbani kwa wazazi wa Kiba ambapo napo anaamini hapafanani na maisha ya mkali huyo wa Bongo Fleva.
“Nyinyi najua mnaweza kufanyia kazi habari hii, nendeni pale Kariakoo nyumbani kwa baba yake Kiba halafu mtaniambia,” alisema.
Amani liliingia mzigoni kujiridhisha na zengwe hilo ambapo hata hivyo, lilibaini kwamba hoja ya watoa ubuyu hao haikuwa na mashiko sana kwani nyumba hizo zina hadhi kwa maana ya kujengwa kwa matofali ya simenti licha ya kutolingana na za vijana wao.
Uchunguzi wa Amani ulibaini kuwa vijana hao wanajitahidi kuwahudumia wazazi wao wakiwa mjini, kulinganisha na baadhi ya vijana ambao wapo mjini na wazazi wao wanaishi katika mazingira ya hali duni kijijini.
Licha ya upande wa baba Diamond mwanaye kudaiwa kutompa mahitaji muhimu kwa sasa lakini hata hivyo, mzazi huyo amekuwa akijikwamua kwa vibiashara vyake pamoja na kuchukua kodi kwa baadhi ya wapangaji aliowapangisha.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa vijana wengi (wakiwemo mastaa) wanapofanikiwa, huanza kujijenga wao kwa kumiliki nyumba na magari ya kifahari kabla kuboresha maisha ya wazazi wao.
Aidha, baadhi ya wazazi nao wamekuwa wakishinikiza watoto wao kufanya mambo makubwa yanayowahusu kabla ya kuwageukia wao, hiyo ikitajwa kuwa ni faraja kwa wazazi kuona watoto wao wanafanikiwa.
“Unajua kuna watu walitarajia kuwaona Kiba na Diamond wakiwajengea mijumba wazazi wao, hicho ni kitu kigumu kwa Bongo. Kwanza inawezekana wazazi wenyewe wanafurahia kuishi maisha yao ya kawaida huku wakiona raha kuona watoto wao wanafanikiwa.
“Kuna vijana wengi sana mijini wanaishi kwenye nyumba za maana mijini. Wanavaa nguo za gharama lakini wanaishia kuwatumia wazazi wao pesa za matumizi na wazazi wanaona ni sawa.
“Somo kubwa ni kwamba, sisi ambao wazazi wetu wako hai tunatakiwa kuwafanya waishi maisha mazuri kulingana na uwezo wetu, usile vinono wakati wazazi wako wanashinda njaa, usiishi kwenye nyumba ya kifahari wakati wazazi wako wanaishi kwenye nyumba ya nyasi, usitembelee gari la kifahari wakati wazazi wako wanatembea kwa miguu tena umbali mrefu,” anasema mshauri wa masuala ya kimaisha, Salum Kid wa jijini Dar.
Stori: Memorise Richard na Neema Adrian Amani
Diamond na Ali Kiba Waibuliwa Zengwe Kuhusu Makazi Duni ya Baba zao
June 29, 2018
Tags