Diamond amesema hayo leo Juni 19 jijini Dar es salaam alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa chaneli ya Wasafi katika king’amuzi cha StarTimes, Diamond ambaye ni kiongozi wa WCB amesema wanajipanga kuona tamasha hilo linabadilisha maisha ya wasanii nchini.
Amesema tamasha hilo halina lengo la kuua wala kushindana na lingine lolote zaidi ya kuongeza nafasi kwa wasanii kupata nafasi ya kufanya kazi.
“Tamasha hili litakuwa likifanyika kila mwaka ila nitahakikisha kila msimu unapokwisha wasanii wanakwenda mapumziko nje ya nchi au wanaanzisha miradi kutokana na malipo mazuri nitakayowapa,” amesema Diamond.
Aidha ili kufanikisha tamasha hilo, wanazungumza na wafadhili kuhakikisha wasanii wanapata fedha za kutosha zitakazobadilisha maisha.
“Tunaziomba kampuni zituunge mkono vijana kwa kufadhili tamasha hili ili iwe chachu kwa vijana wetu kupata malipo au kipato kitakachokimu maisha yao” amesema.
Kwa upande wake meneja wa WCB, Tale maarufu kama Babu Tale amesema wamedhamiria kukuza sanaa na kuweka heshima kwa wasanii maana ilizoweleke kuona wasanii wanafanya matamasha maisha yao yanabaki vilevile na wachache ndio wananufaika.