Msanii wa muziki Bongo, Alikiba amefunguka ni kwanini hadi sasa kinywaji chake, Mo Faya hadi sasa hakijaingia mtaani/sokoni kama alivyotangaza hapo awali.
Muimbaji huyo anayetamba na ngoma ‘Mvumo wa Radi’ ameiambia Shilawadu, Clouds TV kuwa wameshindwa kuingiza sokoni bidhaa hizo kutokana na kuugua kwa Ommy Dimpoz ambaye ndiye balozi. “Mo Faya zilitakiwa ziingia mtaani toka Idd lakini tumepata mtihani kidogo, mtihani tulioupata ni kwamba balozi wetu (Ommy Dimpoz) anaumwa sana, nasikitika kusema hivyo kwa sababu hali yake si nzuri lakini kila siku kunakuwa na uhafadhali, ndio ninachosubiriwa,” amesema. “Hali yake ikiwa sawa wakati tunazitambulisha anatakiwa awepo. Tunahitaji hali yake iwe sawa, tunatamani awepo,” ameongeza Alikiba.
Ommy Dimpoz kwa sasa yupo katika matibabu nchini Afrika Kusini ambapo alifanyiwa upasuaji wa koo.
Katika hatua nyingine Alikiba amekanusha taarifa zilizobai kuwa bidhaa hizo zimezuiwa kuingia sokoni kutokana na brand yake kufanana na bidhaa nyingine. Kinywaji cha Mo Faya kilitambulishwa kwa mara ya kwanza April 29, 2018 ambayo ilikuwa siku ya harusi ya Alikiba.