Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amemkingia kifua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujibu swali kuhusu Serikali kulipa siku 10 Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka wake wa Pasaka uliotolewa Machi 24, 2018, ambao mbali na masuala ya kiroho, ulitaja changamoto tatu za kijamii.
Swali kuhusu KKKT iliyoandikiwa barua ya kutakiwa kufuta waraka huo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, limeulizwa leo Alhamisi Juni 7, 2018 katika kipindi cha Maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu na mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia.
Katika swali lake, Mbatia ametaka kujua ukweli kuhusu barua hizo lakini baada ya kumaliza kuuliza swali hilo, Dk Tulia amesema haliwezi kujibiwa na kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni.
“Kuna barua wamepewa KKKT na TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ) wakitakiwa kufuta nyaraka zao za Kwaresima,” amesema Mbatia na kuitaka Serikali kueleza uamuzi huo una lengo gani.
Mara baada ya swali hilo, naibu spika huyo amesema, “mtakumbuka mheshimiwa Kubenea (Saed-mbunge wa Ubungo-Chadema) alimuuliza waziri Mkuu swali linalohusu dini na mheshimiwa Spika alizuia suali hilo lisijibiwe.”
Baada ya maelezo hayo, Dk Tulia alimuita mbunge mwingine kuuliza swali huku Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi akiketi na kuzungumza na na wabunge wengine wa vyama vya upinzani chini kwa chini.