Fifa Yaonya Kadi England, Ubelgiji

Fifa yaonya kadi England, Ubelgiji
WAKATI mechi ya kufunga hatua ya makundi katika Kundi G, kati ya England na Ubelgiji leo ikionekana kuwa ya kutegeana zaidi kila timu ikitaka kumaliza nafasi ya pili, tayari Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limeonya licha ya makocha wa timu hizo kila mmoja kudai lengo lake ni kushinda na kumaliza kileleni.

England na Ubelgiji zinalingana kila kitu, kila moja ikiwa na pointi sita, mabao nane ya kufunga na mawili ya kufungwa.

Hata hivyo, England ipo kileleni kutokana na kanuni mpya ya michuano hiyo mwaka huu, ambayo kama timu mbili zinalingana kwa kila kitu, mshindi huamuliwa kwa kupitia timu yenye nidhamu zaidi.

Kanuni hiyo imeifaidisha England kukaa kileleni kutokana na kuwa na kadi mbili tu za njano wakati Ubelgiji ikiwa na kadi tatu za njano.

Hali hiyo inazifanya timu hizo kama zitatoka sare ya aina yoyote leo, huku pasiwe na timu itakayoonyeshwa kadi, basi England itamaliza kileleni na kuwa na nafasi kubwa ya kukutana na ama Brazil au Ujerumani hatua ya robo fainali jambo ambalo miamba hiyo inataka kulikwepa.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Times, kuna mpango “England itafanya makusudi kuonyeshwa kadi kwa lengo kama mechi itamalizika kwa matokeo sare, ishike nafasi ya pili.”

Lakini chanzo ndani ya Fifa kimeonya kuwa “kitakuwa makini na kuchukua hatua kali kwa mchezaji atakayeonyesha utovu huo wa nidhamu ikiwa ni pamoja na kumuongezea kifungo kwa atayejitakia kuonyeshwa kadi ya njano.”

Hata hivyo, kocha wa Ubelgiji, Roberto Martinez, licha ya kudai atafanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake, amesisitiza anataka kushinda mechi hiyo jambo ambalo aliungwa mkono na kipa Thibaut Courtois.

"Kwangu mimi ni fahari kushinda. Sitaki kurudi England Julai nikiwa na hisia za kipigo. Ni fahari kwa sababu wana wachezaji wengi tunaowafahamu na wao wanatufahamu sana."

Kwa upande wa Kocha wa England, Gareth Southgate, amesema hayupo tayari kuona England ikipoteza dhidi ya Ubelgiji licha ya timu hizo zote kuwa na tiketi mkononi ya 16-Bora.

"Tunataka kuendelea kushinda. Akili yetu ni kushinda kila mechi tunayoweza," alisema.

Kwingineko, katika Kundi H, hali ni tofauti kidogo, licha ya Senegal na Japan kulingana pointi na mabao ya kufunga na kufungwa, kwani zenyewe zilishakutana na leo zitacheza dhidi ya wapinzani tofauti, Colombia na Poland.

Senegal ni timu pekee inayotegemewa kulibeba Bara la Afrika katika michuano hiyo kufutia timu nyingine, Misri, Nigeria, Morocco na Tunisia kupoteza nafasi ya kutinga 16-Bora.

Hata hivyo, Senegal inahitaji sare yoyote ama ushindi dhidi ya Colombia leo ili kutinga 16-Bora.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad