Bondia wa nchini Marekani, Floyd Mayweather ametwaa tena nafasi ya kwanza kwenye orodha ya wanamichezo 100 matajiri zaidi duniani kwa mujibu wa Jarida la kibiashara la Forbes.
Bondia huyo alijipatia kitita cha Dola za kimarekani milioni 275 kufuatia ushindi wake katika pambano dhidi ya Conor McGregor, ambaye ameshika nafasi ya nne katika orodha hiyo.
Mwanasoka nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo ambaye aliongoza orodha hiyo kwa miaka miwili mfululizo ameshuka hadi nafasi ya tatu akipigwa kikumbo na mpinzani wake wa Barcelona, Lionel Messi ambaye ameshika nafasi ya pili.
Katika orodha hiyo hakuna mwanamichezo mwanamke, baada ya mwanamkee pekee aliyekuwepo mwaka jana Serena Williams kuondolewa.
Wanamichezo hao 100 kwa ujumla wao walijipatia Dola za Kimarekani bilioni 3.8 likiwa ni ongezko la 23% kutoka mwaka jana limeeleza Jarida la Forbes, ambapo dereva wa mashindano ya Langalanga kutoka nchini Uingereza Lewis Hamilton akishika nafasi ya 12 na mapato ya dola milioni 51.
Hata hivyo wachezaji wa mpira wa kikapu wamedhibiti orodha hiyo kutokana na kulipwa mishahara minono iliyochochewa na mikataba kati ya Ligi ya NBA na makampuni ya Televisheni hasa matangazo yanayofikia dola bilioni 34.