Kocha Mfaransa Pierre Lechantre hakuwahi kudumu na timu zaidi ya mwaka mmoja, wakati huo Klabu ya Simba nayo imekuwa na kawaida ya kutokudumu na kocha kwa kipindi cha mwaka mmoja au zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Kocha Joseph Omog peke yake ndiye aliyedumu kwa mwaka mmoja na zaidi, Mcameroon huyo aliiweza Simba kurejea kwenye michuano ya kimataifa baada ya kukosa kwa miaka minne, Simba ilianza timua timua ya makocha tangu msimu wa 2011/12.
Uongozi wa Simba ulitangaza kumuajiri Mfaransa Lechantre kuwa kocha wa klabu hiyo akichukua mikoba ya Mcameroon Joseph Omog aliyetimuliwa katikati ya msimu uliopita wa 2017/18, lakini taarifa ni kuwa huenda Mfaransa huyo akafungashiwa vilago Simba baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na uongozi.
Kwa mujibu wa Mtandao wa www.transfermark.hezrog.kr.com unaojihusisha na kutoa takwimu za masuala mbalimbali ya michezo umeonyesha kocha Lechantre ana wastani wa kufundisha timu si chini ya mwaka kabla ya kuondoka ama kutimuliwa.
Mfaransa huyo aliwashangaza watu pale alipoamua kuvunja mkataba wake wa kuifundisha timu ya taifa ya Senegar wiki mbili baada ya kukubali kuchukua jukumu hilo mwaka 2012.
Pierre Lechantre alianza kufundisha soka barani Afrika na timu ya taifa ya Cameroon, (Indonitable Lions) kuanzia Januari 1, 1999 hadi Juni 30, 2001 ni sawa na siku (911).