Jaji Mkuu atoa agizo hili kwa Mahakama zote nchini


Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma amewaagiza watendaji wa Mahakama kuanza kutumia mfumo wa Kielektroniki katika ufunguaji wa Mashauri Mahakamani ili kuboresha utoaji huduma,kuongeza uwajibikaji, uwazi na kuondoa mianya ya rushwa na urasimu katika kuwahudumia wananchi. 

Jaji Mkuu Profesa Juma anatoa agizo hilo katika hafla ya kuwatunuku hati za uteuzi Mahakimu wakazi wafawadhi na kuwaapisha Manaibu wasajili wa Mahakama ambapo anasema mfumo huo utakaosimamiwa na msajili mkuu wa Mahakama utasaidia kuondoa malalamiko na kuongeza uwazi zaidi kwenye mhimili huo wa dola. 

Aidha Jaji Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya Mahakimu kujigeuza miungu watu katika utoaji hukumu kwa kivuli cha kutoingiliwa kwa uhuru wa Mahakama na kuwakumbusha uhuru huo usipotumiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni utaingiliwa na mamlaka zingine. 

Kwa upande wao baadhi ya Mahakimu wakazi wafawidhi wateuliwa wanasema mfumo wa Kielektroniki Mahakamani utarahisisha ufuatiliaji wa kesi huku wengine wakiomba mashauri yanayotoka polisi kabla ya kufikishwa mahakamani upelelezi wake ukamilike ili kesi zisikilizwe na kumalizika kwa wakati. 

Kuhusu mhilimili huo kunyooshewa vidole kuhusika na rushwa Mahakimu hao wanasema wamejipanga kuwaelimisha watumishi na watendaji waliopo chini yao kuhusu madhara ya rushwa ili kuendelea kuijengea taasisi hiyo uaminifu kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad