Mamlaka ya Kudhibiti Mawasiliano nchini, TCRA imepiga marufuku kwa vyombo vya habari kupitia maudhui ya mtandaoni ambavyo havina leseni ya kuendesha shughuli hiyo kuweka jambo au taarifa yeyote katika mitandao yao.
TCRA imetoa siku 5 kuanzia leo Juni 11, hadi Juni 15, 2018 kuhakikisha vyombo hivyo vya habari vinakamilisha usajili na kuwa na leseni ya urushaji wa matangazo kupitia mtandao, imesisitiza kuwa kuanzia Juni 15, mwaka huu hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka agizo hilo.
Kufuatia agizo hilo Uongozi wa Mtandao wa Jamii Forums uliojikita katika kuhabarisha umma mtandaoni umeomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza mara baada ya kuamua kutii agizo hilo la kusitisha huduma ya utoaji habari mpaka pale utakapokamilisha usajili huo.
Katika ukurasa wa mtandao huo, JamiiForums wameandika;
”Kutokana na notisi iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Juni 10, 2018 inayotoa muda mfupi wa kututaka kusitisha utoaji huduma mara moja kabla ya Juni 11, 2018, tunalazimika kutii mamlaka na hivyo huduma hii haitapatikana kwa muda wakati tukifanya jitihada za kuhakikisha huduma inarejea.
"Tunasikitika kuwa tunalazimika kufikia hatua hii ghafla lakini ni matumaini yetu kuwa wateja wetu mtaendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki”