Mkongwe wa hip hop Bongo, Jay Moe amefunguka na kudai nidhamu ndio kitu kikubwa kilichosababisha wasanii wengi kupoteza kwenye 'game' wakiwemo wakongwe hata wa sasa wanaojiita kizazi kipya.
Jay Moe ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha 5SELEKT kilichorushwa mubashara Juni 06, 2018 na kusema kilichomsababisha yeye kudumu katika muziki mpaka hii leo licha ya kuwa mkongwe ni nidhamu yake ambayo anaionesha kwa kila mtu ambaye anamzunguka kwa kuwa alishawahi kuona madhara yake.
"kwenye kila kitu unachotaka kidumu kwa muda mrefu ni lazima uwe na nidhamu, katika 'game' yangu walikuwa wasanii wengi ambao walikuja kwenye zama zangu na wakapata umaarufu mkubwa kuliko mimi lakini labda nidhamu yao na kile wanachokifanya ndicho kilichowaangusha", amesema Jay Moe.
Pamoja na hayo, Jay Moe ameenedelea kwa kusema "ninachoshukuru nipo na mahusiano mazuri na watu ambao ninawahitaji kama 'media', mashabiki pamoja na watu wa kwenye muziki 'industry' na hicho ndio kitu kikubwa kwasababu unaweza leo ukawa maarufu halafu ukawa ulishawahi kuwadharau watu wengine hata ikitokea ukawa na shida hawataweza kukusaidia".
Kwa upande mwingine, Jay Moe amesema jambo jingine linalowatesa wasanii wengi wakongwe ni kutotaka kukubali mabadiliko ya muziki ili waweze kuendana na soko jinsi linavyotaka kwa sasa nasio kuendelea kufanya kazi kizamani.