Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Anastazia Wambura amesema Serikali imepoteza Sh5.98 trilioni kati ya mwaka 2009 hadi 2017, sawa na asilimia 14.51 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18.
Pia, amesema katika kipindi hicho Tanzania imepata hasara ya Sh3.169 trilioni kutokana na mfumo mbovu kwenye bahari kuu.
Akizungumza leo Jumamosi Juni 2, 2018 katika makabidhiano ya taarifa za kamati mbili za kuchunguza uvuvi wa bahari kuu na gesi, Wambura amesema hatua ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusitisha utoaji wa leseni za meli za kigeni ulisababisha hasara ya Sh5.4 bilioni katika kipindi cha 2016/17.
Amesema mbali na hasara hiyo, Taifa limekuwa likipoteza Sh352 bilioni kila mwaka kutokana na kuuza samaki ghafi nje ya nchi.
Katika taarifa yake hiyo, Wambura amesema hatua ya kutokuwa na bandari ya uvuvi kumeisababishia Serikali hasara ya Sh31.2 bilioni katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2017.
Amesema kiuhalisia sekta ya uvuvi inaweza kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi, lakini Taifa halinufaiki kutokana na changamoto walizobaini.