Kansime Atoboa Siri Jinsi Pesa Ilivyovunja Ndoa yake


Sababu nyingi zimeelezwa kuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa ya mchekeshaji maarufu Afrika Mashariki, Anne Kansiime na aliyekuwa mumewe Gerald Ojok.

Wapo waliosema fedha, kushindwa kubeba ujauzito au kuchepuka. Tetesi hazijawahi kuacha kusikika kila kona, lakini mwenyewe ameibuka na kukata mzizi wa fitina.

Katika mahojiano yake mwishoni mwa wiki iliyopita, Kansiime alifunguka kwanza kukiri kuvunjika kwa ndoa hiyo akisema anatangaza nafasi kwa mwanamume aliye tayari kuwa naye.

Mtangazaji alipomuuliza sababu ya kuvunjika kwa ndoa yake alisema hana uhakika ila anahisi suala la kipato linaweza kuwa limechangia.

“Mimi nilikuwa naingiza fedha nyingi kuliko yeye, huenda hiyo ni sababu lakini sina uhakika,” anasema.

Katika mahojiano hayo pia alitoboa kuwa ndoa yake ilivunjika muda mrefu lakini alikuwa akiogopa kuwaambia mashabiki wake na watu wa karibu akihofia kuonekana mwanamke mpumbavu.

“Kusema ukweli ndoa yangu ilivunjika miezi sita kabla dunia nzima haijajua. Nilificha nikijipa muda wa kutafakari namna nzuri ya kuwaeleza mashabiki wangu. Niligundua kuwa najiumiza bure kwa sababu sasa nipo huru,” alisema.

Kansiime ni mchekeshaji ambaye amejizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki kwa uwezo wake wa kuweka utani kwenye maisha ya kawaida.

Pia alijipatia umaarufu kupitia mitandao ya kijamiii ambako alianza kwa kuweka vipande vya video akiigiza kama mwanamke wa Kiafrika anayekutana na changamoto mbalimbali za maisha.

Mchekeshaji huyo wa kike, ambaye pia huendesha kipindi cha “Don’t Mess With Kansiime” kwenye kituo cha Citizen TV, anatajwa kuwa mwanamke mwenye kipaji cha pekee nchini Uganda na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad