Katibu Mkuu NECTA Ashambuliwa na Wananchi


Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde ameshambuliwa na kujeruhiwa na wananchi baada ya gari alilokuwa amepanda kugonga pikipiki na kusababisha kifo cha dereva.


Tukio hilo lilitokea juzi saa kumi jioni katika Kijiji cha Inala, Kata ya Ndevelwa katika Manispaa ya Tabora.


Dk Msonde amesema anaendelea vizuri na kwamba ajali ilitokea akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi.


“Ninaendelea vizuri. Haya maumivu ninayoyasikia yanatokana na kipigo kutoka kwa wananchi waliotuvamia baada ya ajali ile kutokea,” alisema Dk Msonde.


Hata hivyo, katibu mtendaji huyo hakuwa tayari kueleza kwa kina chanzo cha ajali na namna walivyoshambuliwa. “Naomba itoshe kusema ninaendelea vizuri.”


Ofisa habari wa Necta, John Nchimbi alisema Dk Msonde aliruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kidete jana alikokuwa akipatiwa matibabu.


Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tabora, Nestory Didi alisema gari alilopanda Dk Msonde lilimgonga Mzee Salum (23) alipokuwa akikata kona kuingia nyumbani kwake.


Alisema kutokana na ajali hiyo wananchi walifanya vurugu ndipo dereva alipokimbia na kumwacha Dk Msonde.


Didi alisema Dk Msonde alitibiwa na kuruhusiwa na hakuwa na madhara makubwa mwilini kama baadhi ya watu wanavyodai.


Kamanda huyo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake waache sheria ichukue mkondo wake.


Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad