"Katika Kipindi Hiki Hakuna Kitu Kinachoitwa Silaha ya Siasa ni Nguvu ya Hoja na Weledi kwa Kuwa Hoja hizo Zinapigwa kwa Silaha za Vita" Tundu Lisu
0
June 02, 2018
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amefunguka na kumkosoa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo kuwa katika kipindi hiki hakuna kitu kinachoitwa silaha ya siasa ni nguvu ya hoja na weledi kwa kuwa hoja hizo zinapigwa kwa silaha za vita.
Lissu ametoa kauli hiyo leo Juni 2, 2018 baada ya kupita takribani siku tatu tokea Katibu Mkuu Kitila kutoa kauli yake iliyokuwa inampongeza Dkt. Bashiru Ally kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya ndani ya CCM iliyokuwa ikisema 'katika kipindi ambacho silaha ya siasa ni nguvu ya hoja, weledi, na uimara wa kiitikadi, CCM imepata katibu mkuu sahihi kwa zama sahihi. Nakutakia mafanikio makubwa Comrade Dkt Bashiru Ally'.
"Profesa Kitila Mkumbo hiki sio kipindi ambacho 'silaha ya siasa ni nguvu ya hoja, weledi na uimara wa kiitikadi. Badala yake, hiki ni kipindi ambacho siasa za nguvu ya hoja zinapingwa kwa hoja ya silaha za vita - risasi, mabomu, utekaji nyara na magereza....
Hiki ni kipindi ambacho msimamo wa kisiasa na weledi wa kitaaluma unanunuliwa kwa pesa au kwa vyeo au kwa madaraka. Ni kipindi ambacho umalaya wa kisiasa na kitaaluma umeshamiri na unazawadiwa hadharani badala ya kukemewa na kukataliwa", amesema Lissu.
Pamoja na hayo, Lissu ameendelea kwa kusema "ni kipindi cha giza nene kwa utu na haki za binadamu, kinachotukumbusha zaidi yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaani, utesaji na mauaji ya kisiasa ya akina Abdullah Kassim Hanga, Othman Shariff, Abdul Aziz Twala, Saleh Saadalla Akida, Mdungi Ussi na wengineo wengi".
Kwa upande mwingine, Lissu amedai kipindi hiki ni cha aibu kubwa kwa nchi ya Tanzania hasa kwenye zama hizi za mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Facebook Twitter
Tags