Awali moja ya timu ambazo zilikuwa zinapewa nafasi kubwa na mashabiki ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo, Yanga ilikuwepo.
Ni ngumu kushindwa kuitaja Yanga kwenye michuano kama hii kwa kuwa ni kati ya timu kubwa hapa nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Yanga ina heshima yake, Yanga ni timu kubwa ndiyo maana ipo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, huwezi kuepuka kuipa sifa yake.
Lakini kinachotokea Yanga sasa kinaonekana kuanza kuzoeleka, imeshakuwa kawaida kwa Yanga kufungwa sasa, mashabiki nao wameonyesha kama vile wameanza kuzoea hali hiyo.
Kama Yanga ikishinda mchezo kila mmoja anashangaa na atakuuliza imekuwaje wakashinda? Hii ni kwa kuwa imekuwa ni kawaida kwao kufungwa.
Siku chache kabla ya kwenda Kenya, Yanga walichapwa mabao 3-1 na Azam, juzi tena wamechapwa mabao 3-1 na Kakamega, timu ambayo ilikuwa haipewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
Lakini ukiitazama Yanga uwanjani, mashabiki jukwaani utakubaliana nami kwamba walikuwa wanasubiri kufungwa tu na siyo jambo lingine.
Yanga wakifungwa bao moja wanasubiri kufungwa lingine, hawana wachezaji wanaojali, lakini hata wale ambao wapo uwanjani wanaona kawaida hata kama wakipoteza kwa kuwa naamini hata kocha huwaambia tumefungwa kwa kuwa hatuna fedha.
Hii ni kauli mbaya sana, kwa Yanga na itawatafuna kwa muda mrefu sana, kauli yao wanatembea nayo kwa sasa ni kuwa “Sisi ni maskini, Yanga haina hela”.
Sasa Yanga wanafungwa hata na Mbeya City wanasema hawana hela, ni kweli kuwa Yanga na Mbeya City kigezo kinakuwa na fedha? Siyo kweli.
Yanga ukiwatazama uwanjani unamuona mchezaji mmoja tu anayejituma, Papy Tshishimbi, je huyu ana fedha? Au analipwa mshahara na TP Mazembe? Hapana analipwa na Yanga, lakini anajituma mpaka wakati mwingine unaweza
kufikiri anafanya mazoezi na timu nyingine.
Hakuna sura ambayo inaonekana kukasirika kutokana na matokeo wanayopata Yanga kwa sasa, kila mmoja anaona kawaida tu.
Hii inaonyesha kuwa kupoteza mchezo kwao ni jambo la kawaida kabisa ndiyo maana hata ukimsikia kocha wao, Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila wakiwa wanazungumza kuhusu kupoteza mchezo wanaongea kawaida kwa kuwa wameshaaminishwa kuwa Yanga haina hela hivyo haiwezi kushinda, upuuzi.
Kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Kakamega jukwaani walikuwa wanaonekana baadhi ya mashabiki ambao wametoka Tanzania kwenda kuishabikia timu yao wakiwa wanalia baada ya dakika tisini kumalizika na Yanga kuchapapwa mabao 3-1, hii inaonyesha kuwa wenyewe wanaumizwa na kile kinachotokea sasa kwenye timu hiyo, lakini ni kweli kuwa makocha na wachezaji wanalia kama hawa mashabiki, sidhani naona kwao ni kawaida kufungwa kwa kuwa wana kauli yao “Hatuna fedha”.
Nani anaweza kuwafuta machozi hawa mashabiki waliotumia fedha zao kuifuta timu nchini Kenya halafu ndani ya dakika 45 tu, Yanga ilishaondolewa kwenye michuano hii tena kwa aibu.
Wengine wameacha familia zao bila chakula cha kutosha kuifuta Yanga, watalipwa na nani, wameacha watoto wao hawajamaliza kulipa ada nani atawalipa na bado wanatoa machozi jukwaani.
Kuna kiongozi au mchezaji wa Yanga ambaye alilia baada ya kuona timu hiyo imepoteza mchezo wa juzi kama wale mashabiki jukwaani au walienda kwenye vyumba wakasema Yanga haina fedha?
Mashabiki wapo na Yanga sasa, wale wanaotaka kuwa viongozi kwenye timu hiyo nao wapo wapi, wale wanaotaka kugombea uenyekiti kwenye timu hiyo wapo wapi, mbona hawafanyi kazi sasa?
Kama kuna kipindi ambacho Yanga wanahitaji kufarijiwa ni sasa, kama kuna kipindi ambacho Yanga wanahitaji msaada ni sasa ambapo wanategeneza timu yao, lakini kama kuna kipindi ambacho mtu angepata uongozi bila jasho kubwa ni sasa.
Mashabiki wa Yanga sasa ndiyo wanatakiwa kufahamu nani ndugu yao, nani anaweza kuwasaidia, nani siyo ndugu yao, wale mashabiki wanafaa kuwa viongozi Yanga kuliko bosi anayetoka ofisini amevaa suti.
Yanga sasa wanatakiwa kushikamana na kuonyesha kuwa wanaweza wakati mwingine kung’ang’ania madaraka kama mambo hayaendi ni jambo baya, kama viongozi wa Yanga wanaona hakuna mwanga mbele ni vyema wakajiuzulu na kuwapa nafasi wengine, labda watawafuta machozi mashabiki wao waliokwenda Kenya.
Kwa mwenendo wa Yanga kwa sasa ni hakika inahitajika akili mpya, inahitaji watu ambao wanaweza kulia baada ya kupoteza mchezo na siyo wanaokwenda vyumbani wakisema hatuna fedha.