Serikali imesema walimu wote waliohamishwa kabla ya tamko la Rais John Magufuli aliyeagiza wote wanaohamishwa kupewa kwanza stahiki zao, watalipwa fedha zao kwa kuwa madai yao ni halali.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 25, 2018 bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Joseph Kakunda wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo.
Katika swali lake Susan alitaka kujua ni lini walimu waliohamishwa watalipwa madai yao ikiwemo waliobadilishiwa vituo vya kazi kutoka ualimu wa sekondari na kuwa walimu wa shule za msingi.
Akijibu swali hilo, Kakunda amesema zoezi la kuwahamisha walimu kabla ya kupewa malipo lilisitishwa baada ya kauli ya Rais hivyo madeni yaliyopo ni waliokuwa wanahamishwa bila malipo na kwamba baada ya tamko la Rais, hali ni nzuri.
Awali mbunge wa Mbagala (CCM), Issa Mangungu alihoji ni kwa nini Serikali ilifuta posho za kufundishia na lini itazirudisha ili kuwatia moyo walimu waweze kufundisha zaidi.
Naibu Waziri amesema posho hiyo haikufutwa bali iliongezewa katika mishahara ya walimu kwa lengo la kuongeza mishahara na pensheni wakati wa kupata kiinua mgongo.