Jeshi la Polisi mkoani tabora linamshikilia Kadege Thabit (18), mkazi wa Utemini wilaya ya Uyui mkoani hapa kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa mwaka mmoja na miezi miwili kutokana na imani za kishirikina
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo na kumwingilia kinyume cha maumbile.
Kamanda Mutafungwa ameeleza kwamba mtuhumiwa alitenda tendo hilo baada ya kumchukua mtoto huyo kutoka kwa mama yake akidai anaenda kumnunulia maandazi.
Ameongeza kuwa mtuhumiwa baada ya kumnunulia maandazi mtoto huyo alimpeleka chumbani kwake akafunga mlango ndipo akatenda unyama huo.
“Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la polisi umebaini kuwa sababu za kufanya ukatili huo ni imani za kishirikina, na kwamba uchunguzi zaidi wa tukio hilo bado unafanyika,” amesema
Kamanda Mutafungwa amefafanua kwamba mtuhumiwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa alidai kuwa alitenda kosa hilo kutokana na maelekezo ya mganga mmoja wa kienyeji kwamba ataweza kupata mali nyingi.