UONGOZI wa Klabu ya Yanga umeibuka na kuweka wazi kwamba umewapiga pini wachezaji wake wote kwa kutosajiliwa na timu nyingine za hapa nchini na ikitokea timu ambayo itamsajili nyota wao basi wao watakuwa wamemruhusu mchezaji huyo kufanya hivyo.
Viongozi wa klabu hiyo wapo kwenye mpango wa kuhakikisha wanawazuia wachezaji wao wengi ambao mikataba yao imefika ukingoni wakiwemo Obrey Chirwa, Hassan Kessy na Andrew Vicent ‘Dante’.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, amesema kwamba licha ya wachezaji wao kumaliza mikataba lakini wanafanya kila hali kuhakikisha kwamba hawasajiliwi na wapinzani wao kutokana na kuwepo kwenye mipango ya kuwatumia katika msimu ujao wa ligi kama ambavyo walivyoambiwa na kocha wa timu hiyo Zahera Mwinyi.
“Licha ya kwamba kuna wachezaji wengi ambao wamemaliza mikataba hapa kwetu lakini tuseme tu tumejiandaa kikamilifu kuona kwamba wanasalia hapa na kucheza kwa msimu ujao kwa sababu kocha anawataka waendelee kubaki kwa ajili ya msimu ujao na michezo ya kimataifa.
“Tunaendelea na mazungumzo na kila mchezaji ambaye amemaliza mkataba ili awepo na sisi lakini ukiona kwamba mchezaji wetu amesajiliwa na timu nyingine yoyote ile basi tambua kwamba tumempa ruhusa ya kufanya hivyo, ila kama siyo basi sura zote zitaendelea kuonekana katika jezi zetu kwa msimu ujao,” alisema Nyika.
Simba walikuwa wanaelezwa kuwa wanamtaka mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa na Papy Tshishimbi kwenye dirisha hili la usajili na hivyo sasa wakiwahitaji lazima waongee na Yanga.