KKKT Yatakiwa Kufuta Waraka Ilioutoa Wakayi wa Pasaka
0
June 06, 2018
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeelekezwa kufuta waraka lililoutoa wakati wa Pasaka Machi 24 ambao mbali ya masuala ya kiroho, ulitaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini.
Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.
Katika mitandao ya kijamii leo Juni 6, 2018 imesambazwa barua inayoonyesha imeandikwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa mwenyekiti /askofu mkuu wa KKKT iliyoandikwa
Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.
Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.
“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’. Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.
Mwananchi inaendelea kufuatilia kwa wahusika kuhusu barua hiyo na tutaendelea kutoa habari.
Tags