KOCHA Mkuu wa Singida United, Hemed Morocco, ametoa kauli ya kishujaa kwa kusema kuwa, licha ya Simba kuendelea kufanya usajili mkubwa, lakini hawaihofii wakikutana kwenye michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza leo Ijumaa jijini Dar.
Simba ambayo inaendelea na usajili, hivi karibuni ilitangaza kumsajili Meddie Kagere kutoka Gor Mahia ya Kenya ambapo kwenye Kagame, Simba na Singida zimepangwa kundi moja la C.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Morocco alisema kwa mwaka huu wanataka kushinda kila kitu, hivyo wanaanza na Kagame.
“Tunataka kushinda kila kitu, hayo ndiyo malengo yetu na ndiyo maana tuko watulivu katika usajili.
“Tunataka kutumia mashindano ya Kagame kwa mambo matatu, kwanza kushinda kila mechi na kutwaa ubingwa, pili ni nafasi ya wachezaji wetu kupata uzoefu wa mechi kubwa, na tatu ni kupata muunganiko mzuri wa wachezaji wetu kabla ya kuanza kwa ligi.
“Tupo kundi moja na Simba, wala hatuihofii, tumejipanga kupambana nayo na timu nyingine zote tutakazokutana nazo,” alisema Morocco.