Kubenea Amuomba Rais Magufuli Amuajibishe Mutungi

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amemuomba Rais John Magufuli kumuwajibisha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa madai kuwa ameshindwa kutimiza wajibu wake.

Leo katika mkutano wa wabunge wa Ukawa  Kubenea ameyasema hayo wakati akizungumzia hatima ya ruzuku za CUF, kufuatia ofisi ya msajili kuendelea kutoa ruzuku ya chama hicho kwa upande wa Prof. Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho anayejulikana na Msajili wa vyama, bila kujali zuio la mahakama.

Amesema kitendo kinachofanywa kwa sasa na Jaji Mutungi ni sawa na kuibaka demokrasia, na kwamba haikubaliki kkwa kuwa kinachafua uso wa Tanzania kimataifa.

“Huyu Mutungi ni hatari hapaswi kuachwa aendelee kwani amepoteza sifa na anaonekana kuwa na maslahi flani. Haiwezekani jambo hili likawa linatokea na Rais anaangalia bila ya kulifanyia kazi" Kubenea.

Tangu mwaka 2016  Chama cha CUF kilijikuta kikiingia kwenye mgogoro baada ya Profesa Lipumba kutaka kurejea katika nafasi yake ya uongozi (Uenyekiti wa Chama) ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipoandika barua ya kujiuzulu.

Mapema leo viongozi wa CUF upande wa Katibu Mkuu Maalim Seif walibainisha kuweza kuzuia kutolewa kwa kiasi cha sh. Mil 600 kwenye akaunti ya Lipumba baada ya kuingiziwa fedha hizo na Msajili wa Vyama vya siasa kinyume na agizo la mahakama.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad