Kubenea Amwomba Rais Magufuli Kumuwajibisha Jaiji Mutungi "Huyu Mutungi ni Hatari Apaswi Kuachwa Amepoteza Sifa"

Kubenea Amwomba Rais Magufuli Kumuwajibisha Jaiji Mutungi "Huyu Mutungi ni Hatari Apaswi Kuachwa Amepoteza Sifa"
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amemuomba Rais John Magufuli kumuwajibisha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa madai kuwa ameshindwa kutimiza wajibu wake.

Kubenea ametoa kauli hiyo leo Juni 11, 2018 katika mkutano wa wabunge wa Ukawa waliozungumzia hatima ya ruzuku za CUF, kufuatia ofisi ya msajili kuendelea kutoa ruzuku ya chama hicho upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, bila kujali zuio la mahakama.

CUF kimekumbwa na mgogoro tangu mwaka 2016 baada ya Profesa Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kurejea katika uongozi ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipoandika barua ya kujiuzulu. Mgogoro huo umesababisha kufunguliwa kesi mahakamani.

Amesema kitendo kinachofanywa kwa sasa na Jaji Mutungi ni sawa na kuibaka demokrasia, hakikubariki kwa maelezo kuwa kinachafua uso wa Tanzania kimataifa.

“Haiwezekani jambo hili likawa linatokea na Rais anaangalia bila ya kulifanyia kazi. Huyu Mutungi ni hatari hapaswi kuachwa aendelee kwani amepoteza sifa na anaonekana kuwa na maslahi furani,” amesema Kubenea.

Mbunge wa Malindi Ali Saleh (CUF) amesema msajili wa vyama ndio chanzo cha mgogoro ndani ya chama hicho kwa kuwa anafanya mambo kinyume hata na maagizo ya mahakama.

Saleh amesema Msajili alitumia ujanja kukataa kupokea zuio la mahakama kuhusu ruzuku katika kesi namba 80 ya mwaka 2018 lililotolewa Mei 29, 2018 ili atoe kwanza fedha hizo, huku akipongeza uamuzi wa mahakama kutoa zuio wakati fedha zikiwa hatua ya mwisho kutolewa katika moja ya tawi la benki moja jijini Dar es Salaam.

Amesema kitendo cha kukataa hukumu ya mahakama ni kosa kisheria na kuhoji ujasiri anaoupata msajili huyo.

Naye mbunge Mchinga (CUF) Hamidu Bobali amesema msajili amesharuhusu Sh600 milioni kuingizwa katika akaunti ya wilaya ya chama hicho,  lakini uongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho walibaini jambo hilo na kuzizuia.

Amedai fedha hizo zilikuwa maalum kwa ajili ya kuendesha mkutano wa chama hicho uliopangwa kufanyika mkoani Singida.
Chanzo: Mwananchi

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad