Kubenea Awapigania Wanaume Wenye Wake Zaidi ya Mmoja

Kubenea Awapigania Wanaume Wenye Wake Zaidi ya Mmoja
Serikali  inaangalia namna ya kuhakikisha wanaume wenye wake zaidi ya mmoja wanaingiza wenzi wao hao kwenye huduma ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Ahadi hiyo ilitolewa jana bungeni jijini hapa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda.

Kakunda alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema).

Katika swali hilo, Kubenea alihoji kwa kuwa NHIF inatambua mke mmoja, serikali ina mpango gani kuruhusu wake wawili kuingizwa kwenye mfuko huo tofauti na ilivyo sasa.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika, naibu waziri huyo alisema serikali inatambua kuwa wananchi wake wana dini ambapo moja -kiislam - inaruhusu kuoa mke zaidi ya moja.

Alisema kutokana na ukweli huo, itaangalia namna ya kulifanyia kazi suala hilo.

“Serikali tunatambua kuwa wananchi wana dini na inaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja, acha tulichukue ili kulifanyia kazi,” alisema Kakunda.

Mbali na kuingizwa mke wa pili, naibu waziri huyo aliahidi pia kuangalia uwezekano wa bima hiyo kuwakinga pia wazazi wa mwanachama.

Huduma za NHIF kwa wanachama zinahusu pia wenza na watoto wasiozidi wanne na walio chini ya umri wa miaka 18, vinginevyo wawe wanasoma.

Kwa watoto wanaosoma, ukomo wa huduma hiyo ni pale watakapotimiza umri wa miaka 21.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad