MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, jana Jumanne alikabidhi msaada wa aina mbalimbali kwa watoto yatima ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sikukuu ya Idd ambayo inategemewa kuwa Ijumaa au Jumamosi wiki hii.
Sirro alitoa msaada huo uliojumuisha mafuta ya kula, mchele na miswaki katika sherehe ya futari iliyowakutanisha viongozi mbalimbali katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi (Police Mess) uliopo Oyster Bay jijini Dar.
Katika hafla hiyo ilijumuisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda; Sheikh Mkuu wa Tanzania, Aboubakary Zubeir; Sheikh wa Mkoa wa Dar, Alhad Mussa Salim; Kamanda mstaafu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na viongozi wengine mbalimbali wa dini na siasa.
Mkuu huyo wa polisi alisema: “Nawashukuru wote ambao mmejitokeza hapa, bila ya nyie shughuli hii isingeweza kufanyika. Jambo hili ambalo linatokea hapa kwa nchi nyingine ni ngumu kufanyika kutokana na kukosa amani, hivyo tunatakiwa kushirikiana kwa ajili ya kuitunza amani yetu iliyopo kwani nchini nyingine zinatamani kuwa kama sisi.”