Kumekucha..Deni la Taifa laongezeka kufikia trilioni 49


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amesema mpaka kufikia April 2018 deni la Taifa limeongezeka na kufika trilioni 49.6 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 13.4 ukilinganisha na deni la mwaka 2017 trilioni 43.7.


Waziri Mpango amesema hayo leo Juni 14, 2018 wakati wa kuwasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Bungeni Jijini Dodoma na kusema kuwa deni la ndani ni trilioni 14.05 na deni la nje ni trilioni 35.6 ambapo ni sawa na asilimia 71.7 ya deni lote na kuongeza kuwa deni la serikali linaongezeka kutokana na mikopo ya zamani na malimbikizo ya riba ya deni la nje na kusema kuwa deni hilo ni stahimilivu.

“Mikopo nafuu kutoka mashirika ya fedha za kimataifa imeeendelea kuwa chanzo kikuu cha mikopo kutoka nje ambayo imechangia asilimia 59.6 ya deni lote la nje, mikopo yenye masharti ya kibiashara limechangia asilimia 25.5 na mikopo kutoka nchi wahisani imechangia asilimia 11.9, mikopo hii imetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, deni la serikali limekua likiongezeka, lakini deni hili limeendelea kuwa himilivu”, amesema Waziri Mpango.

Waziri Mpango ameongeza kuwa katika tathimini ya uhimilivu wa deni uliofanyika Novemba 2017 imeonesha uwiano wa deni kwa thamani ya sasa ya pato la taifa ni asilimia 34.4 ambapo ukomo wa deni la Taifa ni asilimia 56.

Katika kupunguza mzigo wa madeni Serikali itatoa kipaumbele kulipa madeni ambayo yanaongezeka kutokana na riba pamoja na madeni yanayogusa watoa huduma wengi wa wakiwemo watumishi, wazabuni na madai ya wakandarasi.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad