Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe amesema kuwa Lugha ya Kiswahili ni moja ya lugha 10 duniani zinazotumiwa na watu wengi kati ya lugha 6000.
“Kwenye vitu vingi tumeshika mkia dunia lakini kwenye hili tupo kwenye 10 bora katika ya lugha 6000,” alisema Waziri Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa kumbukizi ya Shaaban Robert na Tamasha la Ustaarabu wa Mswahili uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Chuo cha Mt. John jijini Dodoma.
Shaaban Robert alikuwa ni mwandishi nguli wa vitabu vyenye maudhui mbalimbali vikiwemo vya Kusadikika, Kufikirika pamoja na Adili na Nduguze, alizaliwa Januari Mosi, 1909 na kufariki June 22,1962.