Rais Dkt. John Magufuli ameagiza shilingi milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara Jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu jana Juni 29, 2018, wakati akizindua kituo cha Polisi kinachohamishika katika hafla iliyofanyika eneo la Kisasa, Jijini Dodoma na kusema Rais Magufuli ametoa agizo hilo ili fedha hizo ziende kukarabati miundombinu ya barabara pamoja na taa za kuongezea magari katika barabara ya kisasa na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya Emmaus-African Dream yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha lami.
"Kutokana na msongamano uliopo ambao unaweza kusababisha ajali. Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Magufuli ameamua fedha zote zilizoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zitumike kuboresha barabara. Pia ameawataka watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi", amesema Waziri Mkuu.
Kufuatia uamuzi huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mkoa waratibu zoezi hilo kwenye maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Polisi lianze kujikita kwenye matumizi ya mifumo ya kiulinzi ya kielektroniki yaani 'City Surveillance Sytems' ili limudu kudhibiti hali ya sasa ya uhalifu.
Kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huadhimisha siku ya mashujaa kama sehemu ya kuwaenzi mashujaa hao ambao waliipigania nchi hii kwa namna moja ama nyingine.