Jopo la Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambapo amelazwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamewapiga marufuku watu kuenda kumtazama Mbowe kwa kile wanachodai kuwa yupo kwenye vipimo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema leo Juni 18, 2018 kupitia mtandao wao maalum wa chama baada ya kupita masaa machache tokea ilipo ripotiwa taarifa ya kiongozi huyo ndani ya Mahakama kuwa ameshindwa kuhudhuria kesi yake kutokana na kuanguka ghafla na kukimbizwa Hospitalini.
"Nimefika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe. Freeman Mbowe, kwa sasa madaktari wameshauri kuwa mgonjwa hataweza kuonwa kwa kuwa yuko kwenye vipimo. Hivyo kwa wale wote ambao walikuwa wamepanga kwenda hospitali kumuona mnaombwa msitishe hadi mtakapopewa taarifa nyingine", amesema Mrema.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema amesema hali ya Mbowe kwa sasa inaendelea vizuri tofauti na alipopelekwa hapo awali.