MADINI ya Tanzanite zaidi ya kilo mbili yenye thamani ya mamilioni ya fedha yameibwa


MADINI ya Tanzanite zaidi ya kilo mbili yenye thamani ya mamilioni ya fedha yameibwa katika mgodi wa kitalu C unaomilikiwa na Tanzanite One na kupitishwa geti la ukuta unaozunguka migodi yote Mererani yanakochimbwa madini hayo adimu wilayani Simanjiro, Manyara.

Madini hayo yameibwa wakati Rais Dk John Magufuli akiwa ameamuru askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujenga ukuta kuzunguka mgodi huo kuthibiti utoroshaji madini hayo serikali iweze kunufaika.

Madini yaliyoibwa yalichimbwa na kuibiwa kwa njia ya wizi maarufu kwa jina la bomu katika mgodi wa kitalu C unaomilikiwa na Tanzanite One na serikali ambapo inadaiwa wachimbaji wadogo wadogo, wana Apollo waliingia kupitia mgodi wa kitalu D wa mfanyabiashara maarufu Arusha (jina tunalo).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga alithibitisha tukio hilo na kusema lilitokea Juni 21, mwaka huu saa 8 usiku na wahusika wamefikishwa mahakamani. Senga alisema suala likishafika mahakamani wao hawawezi kulizungumzia tena lakini wanaendelea kufanya upelelezi zaidi wa tukio.

Vyanzo vya habari Mererani vinadai kuwa kukamatwa wachimbaji hao 11 na wafanyakazi wa Tanzanite One kumeleta sitofahamu kwani kilo moja ya Tanzanite iliyowasilishwa ofisi ya Wizara ya Madini Kanda ya Kaskazini siyo kati ya madini yaliyokamatwa bali Tanzanite nzuri yenye thamani kubwa ndiyo inadaiwa kuibwa.

Vyanzo hivyo vya habari vilidai madini ambayo yalikamatwa zaidi ya kilo mbili yana thamani kubwa na yalipitishwa kirahisi geti kuu la ukuta maarufu kama ukuta wa Rais John Mgufuli.

Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adamu Juma alikiri kupokea madini ya Tanzanite kilo moja kutoka kwa watu waliokamatwa na kuhifadhiwa ofisini kwake. Juma alisema hawezi kutoa taarifa zaidi za wizi huo na madini kupitia getini kwa sasa kwani kuna taarifa nyeti zinatafutwa juu ya tukio hilo.

"Ni kweli nimekabidhiwa madini ya Tanzanite kilo moja ambayo sijui thamani yake kwa sasa kwani walikamatwa nayo wachimbaji wakiiba Tanzanite One,’’ alisema Kamishna huyo.

Habari zinadai wafanyakazi wa Tanzanite One (majina tunayo) ndiyo waliowapora madini wachimbaji wadogo, kuyatorosha, kuyapitisha hadi nje ya ukuta kwenda kuyauza kwa tajiri mnunuzi wa madini Arusha (jina tunalo).

"Madini yaliyopelekwa kwa Kamishina ni mabovu, siyo yale waliowapora wachimbaji kwani wafanyakazi wa Tanzanite One wameiba kwa sababu hawajalipwa mishahara zaidi ya miezi tisa sasa," alisema mtoa taarifa wetu.

Viongozi wa Tanzanite One hawakuweza kupokea simu zao za kiganjani lakini taarifa za ndani zinadai uchunguzi unafanyika ili kujua waliohusika ili hatua zichukuliwe dhidi yao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad