Mafundi Waelezea Upekee wa Jeneza la Pacha Walioungana Maria na Consolata

Mafundi waelezea upekee wa jeneza la pacha walioungana Maria na Consolata
Kitabu cha maisha ya Maria na Consolata Mwakikuti kinafungwa leo watakapozikwa katika makaburi ya Tosamaganga, Iringa vijijini.

Jeneza litakalotumika kuhifadhi miili ya pacha hao walioungana ni la kipekee lililoandaliwa kwa siku nzima ya jana.

Mkurugenzi wa karakana ya Mandela iliyotengeneza jeneza itakamohifadhiwa miili ya pacha hao, Kihwelo Mandela alisema walitumia siku nzima kulikamilisha kutokana na namna lilivyohitaji ufundi wa kipekee.

Fundi mkuu wa karakana hiyo, Oscar Mfugale alisema tofauti ya jeneza hilo na mengine inatokana na vipimo vilivyotumika.

Alisema jeneza la kawaida huwa na upana wa futi 1.5, lakini la akina Maria na Consolata lina upana wa futi tatu.

Mfugale alisema jeneza hilo litakuwa na urefu wa futi tano na kina cha futi mbili, tofauti na la kawaida ambalo kina chake ni futi moja.Padri aliyesimamia ujenzi wa kaburi, Benedict Chavala alisema uamuzi wa pacha hao kwamba wazikwe kwenye makaburi ya Tosamaganga ambako huzikwa viongozi wa Kanisa Katoliki ni wa busara na utasaidia kuendelea kuwaenzi.

“Wakiwa karibu nasi tutawafanyia ibada kila siku, tutawakumbuka kwa sababu ni watoto wetu waliolelewa na masista, hivyo ni busara kuzikwa hapa,” alisema.

Aliwataka ndugu wa pacha hao kuungana na watawa katika kuwaombea kwa kuwa waliyofanya duniani ni ushuhuda.

Sista mkuu wa Shirika la Mtakatifu Teresa, Jimbo Katoliki la Iringa, Kalista Ludega alisema pacha hao watazikwa mahali wanapozikwa masista wa Shirika la Maria Consolata ambalo ndilo limewalea tangu wakiwa wadogo.

Msafara wa mazishi na ving’ora

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa msafara wa mazishi ya pacha hao utaongozwa na gari la polisi na ving’ora.

Alisema waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ndiye ataongoza waombolezaji katika kuaga mwili wa pacha hao.

Viongozi wengine watakaohudhuria, alisema ni naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa, wakuu wa wilaya na mikoa walikowahi kusoma pacha hao.

Pacha hao walisoma Shule ya Msingi Ikonda wilayani Makete walikohitimu darasa la saba. Walijiunga na Sekondari ya Maria Consolata wilayani Kilolo walikomaliza kidato cha nne, na kidato cha sita walihitimu katika Sekondari Udzungwa.

“Tunatarajia viongozi wengine wengi wa kitaifa watakuwa pamoja nasi,” alisema Kasesela.

Kasesela ambaye ni kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa, alisema pacha hao waliofariki dunia Juni 2 katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, miili yao itapelekwa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), saa moja asubuhi kwa ajili ya misa na kuagwa.

Maria na Consolata walikuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo wakisoma shahada ya elimu.

Kasesela alisema misa itaongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa na Askofu Alfred Maluma wa Jimbo la Njombe.

“Kutakuwa na salamu kutoka kwa viongozi kisha msafara wa kuelekea Tosamaganga utaanza saa saba mchana,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika saa nane na nusu mchana.

Kauli ya baba

Asukile Mwakikuti, baba mkubwa wa Maria na Consolata alisema kifo cha watoto hao kimeacha simanzi kubwa kwa familia yao.

Alisema kutokana na malezi bora ya Shirika la Maria Consolata wameridhia watoto wao wazikwe Tosamaganga.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad