Maiti Mbili Zilizookotwa Ubungo Viongozi Watofautiana Maelezo

Maiti Mbili Zilizookotwa Ubungo Viongozi Watofautiana Maelezo
Maiti mbili zilizokutwa katika Manispaa ya Ubungo zimezua utata, baada ya viongozi wa manispaa hiyo kukinzana kuhusu mahali sahihi zilipokutwa.

Miili hiyo ambayo yote ni ya wanaume iliokotwa kwa nyakati tofauti, mmoja asubuhi ya Juni 7 na mwingine jioni ya Juni 12. Kupitia ukurasa wake wa Twitter juzi, meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob aliandika, “Tarehe 7 Juni alfajiri 2018 na tarehe 12 Juni jioni, siku mbili tofauti zimeokotwa maiti mbili za kiume pembezoni mwa lango la ofisi za Manispaa ya Ubungo. Zikionekana kufungwa kamba na kuteswa kisha kutupwa na kutelekezwa nje ya ofisi zetu.”

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Makori Kisare alikiri kutokea kwa matukio hayo, lakini akakanusha kuwa miili haikuokotwa mbele ya lango la ofisi za manispaa.

“Ni kweli tumepata shida hiyo, ila sio kama meya anavyoeleza kwamba ni kwenye lango la ofisi za manispaa. Miili hii imeokotwa pembezoni mwa Barabara ya Morogoro unapokata kona ya kuja kwenye ofisi zetu. Hilo lilikuwa eneo la watu wanafyatua matofali, sasa wameondoka na kuacha shimo ambalo lilijaa maji,” alisema.

Kisare alisema walitoa taarifa kwa vyombo husika na polisi walifika kuitoa miili hiyo na mmoja kati yao umetambulika kuwa ni mkazi wa Kibaha na alikuwa ni dereva wa bodaboda.

“Mtu wa kwanza alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala, mwingine akapelekwa Tumbi na huyu ndiye alitambulika kuwa ni mkazi wa Kibaha anaendesha bodaboda na alikodiwa, sasa mazingira ya kifo chake hayajafahamika polisi wanaendelea na uchunguzi,” alisema.

Kisare alisema walishauriana na kufikia uamuzi wa kuliziba shimo hilo na tayari maji yameshaondolewa ili kiwekwe kifusi.

“Nilimwambia meya sisi tukiwa kama viongozi tunatakiwa kuwa waangalifu na kauli tunazozitoa kwenye umma zinaweza kuzua taharuki,” alisema Kisare.
Chanzo Mwananchi

Akizungumza na Mwananchi, Jacob alisema kwa sasa wafanyakazi wa manispaa na wakazi wanaoishi jirani na zilipo ofisi hizo wameingiwa hofu juu ya matukio hayo.

Alisema licha ya kuwa miili hiyo iliokotwa kwa nyakati tofauti, yote ilikutwa katika eneo moja ikiwa na muonekano unaofanana.

“Suala hili limeleta taharuki maana watu hawaelewi ile miili ni ya akina nani, wametokea wapi na ilikuwaje hadi wamekutwa na masahibu hayo na hata sisi watumishi inatupa wakati mgumu maana haiwezekani miili inatupwa nje ya ofisi, tunaomba polisi ichunguze na itoe taarifa,” alisema Jacob.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Murilo hakupatikana kuzungumzia kuokotwa kwa maiti hao na hatua za kiuchunguzi zinazoendelea.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad