Majibu ya Naibu Waziri Kilimo Dr. Mwanjelwa Kuhusu Kauli ya Mzigo Mzito Mpe Mnyamwezi

Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM) Almas Maige amesema umefika wakati sasa ambapo ule usemi wa mzigo mzito kumpa Mnyamwezi uachwe.

Akizungumza kabla ya kuuliza swali la nyongeza, Mbunge huyo alisema kuwa kituo cha wanyama kazi cha Puge kina mfanyakazi mmoja tu ambapo hawezi kufanya kazi zote peke yake.

“Suala la mzigo mzito tumpe Mnyamwez tuache, wapunguze wabebe wenye mzigo,” amesema Maige akiitaka serikali kukisaidia kituo hicho.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Kilimo, Dr. Mary Mwanjelwa alikiri kuwa ni kweli kituo hicho kina mtumishi mmoja lakini akaongeza kuwa wizara hiyo haihusiki.

Alisema kuwa tayari wizara ya kilimo ilihamishia vituo vyote vya aina hiyo nchini kwenye halmashauri za wilaya.

Alizitaka halmashauri hizo kuvipa kipaumbele vituo hivyo kwa lengo la kusaidia wananchi wa maeneo husika.

Kwa upande wake Mbunge wa Lupa Victor Mwambalaswa (CCM) alitaka serikali kugawa eneo la kituo cha utafiti cha Nkena kwa wananchi.

Alisema kuwa kituo hicho kina eneo la hekari 500 ambazo zinaweza kugawiwa kwa wanakijiji kwa ajili ya kilimo.

Aidha Mbunge huyo alimtaka Naibu Waziri kutembelea jimbo la Lupa na kuwaeleza wapiga kura umuhimu wa tafiti.

Akijibu swali hilo Naibu waziri Mwanjelwa alisema kuwa kituo hicho kinatumia eneo hilo kwa ajili ya utafiti wa zao la tumbaku.

Alisema kuwa hata hivyo bado eneo hilo halitoshi na itakuwa vigumu kwa serikali kuligawa.Mbali ya Lupa alisema kuwa  eneo hilo pia linatumiwa na watalaam wa chuo cha utafiti wa kilimo cha Uyole kilichopo jijini Mbeya.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad