Makachero Kutoka Korea Kaskazini Walinda Kinyesi, Mkojo wa Kim Jong-un

Makachero kutoka Korea Kaskazini walinda kinyesi, mkojo wa Kim Jong-un
Hafahamiki umri wake sahihi na alipokuwa akisoma lugha ya Kiingereza huko nchini Uswisi alikuwa akitumia jina la Pak Un tofauti na analolitumia sasa. Huyo ni Kim Jong-un, kiongozi machachari wa Korea Kaskazini ambaye safari yake ya kutoka Pyongyang kwenda Singapore umbali wa kilomita 4,743 ilijaa mbinu kadhaa za kikachero ikiwamo kubeba vyombo vya kuhifadhi kinyesi na mkojo wake.

Maisha yake ya shule pia yalijaa ukachero hasa kuhusu umri wake, kuna taarifa zinadai alizaliwa Januari 8, 1982, lakini wengine wanaamini alizaliwa Januari 8, 1983. Makechero wa Marekani wao wanaamini alizaliwa Januari 8, 1984. Makachero wa Korea Kusini wao wanaamini alizaliwa Januari 8, 1983. Lakini, rafiki yake mchezaji wa mpira wa kikapu wa Chicago, Dennis Rodman anasema kiongozi huyo alizaliwa Januari 8, 1983.

Choo maalumu

Usalama wa Kim Jong-un ndiyo suala la pekee kwa makachero wa Korea Kaskazini, mbali na kutanguliza ndege mbili za chambo huko Singapore, moja ikiwa na gari lake aina ya limoisine lisilopenya risasi na lenye vioo vya giza, pia wamebeba choo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi kinyesi na mkojo wa kiongozi huyo ili visiangukie mikononi mwa makachero wa Marekani.


Kwa mujibu wa chombo cha habari za Korea Kaskazini, siteChosun Ilbo ni kwamba makechero wa Marekani hasa CIA wanafahamika kwa kukusanya vinyesi na mkojo wa viongozi wanaowafuatilia kwa lengo la kufahamu afya zao, dawa wanazotumia na kujua udhaifu wao kimwili.

Wakati Rais wa Urusi, Mikhail Gorbachev alipotembelea Washington D.C mwaka 1987 aliamua kuweka makazi kwenye ubalozi wa nchi yake badala ya kufikia kwenye makazi rasmi ya viongozi wageni ya ‘Blair House’ yaliyo jirani na Ikulu ya White House.

Mpango huo ulivuruga njama za CIA za kujaribu kukusanya kinyesi cha kiongozi huyo. Njama hizo pia zilishindikana kwa makachero wa MI6 wa nchini Uingereza pale waliposhindwa kukusanya kinyesi na mkojo wake alipotembelea London.

Mwandishi mmoja Jack Anderson aliwahi kuandika kuwa makazi ya ‘Blair House’ pia yana vyoo maalumu vya kukusanya kinyesi na mkojo kwa wanaofikia makazi hayo. Pia, kuna wakati Mfalme wa Misri aliwahi kukumbwa na kadhia hiyo alipotembelea Monte Carlo.

Kachero mstaafu wa Ufaransa, Alexandre de Marenches aliwahi kuliambia jarida la Time mwaka 2001 kwamba maofisa wake walifanikiwa kuingia kwenye chumba cha hoteli aliyofikia kiongozi wa Sovieti Leonid Brezhnev na kufyatua bomba la choo ambapo walifanikiwa kupata mkojo wa kiongozi huyo.

Makachero wa Marekani waliwahi kusafiri na choo maalumu kwa ajili ya Rais George W. Bush alipotembelea Austria mwaka 2006.

Wataalamu wanasema kinyesi kinaweza kutoa taarifa za afya ya muhusika. Daktari naweza kukichunguza kinyesi na kujua afya ya utumbo mpana, afya ya mfumo wa chakula kuanzia tumboni hadi kwenye utumbo mwembamba, vipimo vya magonjwa na pia kujua kama mhusika anatumia dawa.

Matokeo kamili baadaye

Kitu kingine ambacho bado hakijulikani ni muundo wa makubaliano ya kutimiza azma hiyo ya kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea, ikiwapo hofu iwapo Korea Kaskazini itaridhia kuachana na mpango wake wa silaha hizo kwa kiwango ambacho kinatakiwa na Marekani.

Trump na Kim waliwasili mjini Singapore Jumamosi, na wote kwa nyakati tofauti wamekutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, mwenyeji Lee Hsien Loong. Vilevile maofisa waandamizi wa Marekani na wenzao wa Korea Kaskazini wamefanya mazungumzo ya faragha kabla ya mkutano wa kilele uliofanyika jana.

Mkutano wa ana kwa ana baina ya Donald Trump na Kim Jong-un haukuwa kitu kinachofikirika miezi michache iliyopita, wakati viongozi hao walipokuwa wakitoleana maneno makali kuhusiana na silaha za nyuklia.

Ingawa vita vya Korea vilimalizika mwaka 1953, vita kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini inayoungwa mkono na Marekani bado havijamalizika rasmi, kwa sababu ingawa makubaliano yalifikiwa kusitisha mapigano, pande hizo bado hazijasaini mkataba wa amani.

Top Post Ad

Below Post Ad