Baada ya kikao, katika mkutano na waandishi wa habari Waziri Mwakyembe alieleza kuwa Diamond anafaa kuwa balozi wa maadili kutokana na ushawishi alionao kwa sasa.
“Ndio balozi wetu, balozi wa maadili pia, kwa sababu Diamond utake usitake yeye ni balozi wa Tanzania kwa kila kitu na safari hii tumemuomba hata maadili awe balozi wetu” alisema Waziri Mwakyembe.
Kikao hicho kilikuja baada ya nyimbo mbili za Diamond ‘Waka na Hallelujah’ kufungiwa na kuibuka mvutano kati Diamond na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Juliana Shonza. Tuachane na hilo.
Utakumbuka hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustino Mrema alisema msanii wa Bongo Flava anayemfuatilia ni Diamond Platnumz. Hii ni kutoka muziki wake unakosha hadi wazee kwani ni muimbaji mahiri na akisaidiwa ataufikisha mbali muziki wa nchi hii.
“Namfuatilia sana Diamond, ni kijana mdogo, muimbaji mahiri, yaani Diamond asaidiwe naona hatima yake katika maisha yake na nchi yetu atatufikisha mahali pazuri. Kwa muziki wake unakosha roho, hata sisi wazee, mimi naridhika sana,” alisema.
Kamata maneno ya Waziri Mwakyembe; ‘Utake usitake yeye ni balozi wa Tanzania’. Kamata maneno ya Augustino Mrema; ‘Muziki wake unakosha roho, hata sisi wazee’.
Hivyo ndivyo Diamond amelijenga jina lake kwa viongozi wa kiserikali na sio viongozi tu, bali watu wenye umri wa makumu. Je, wale wa rika lake, yaani washikaji zake wanamchukuliaje?.
Rayvanny ambaye ni msanii wa pili kusainiwa katika label ya Diamond, WCB, na pia wameshirikiana katika nyimbo mbili, alieleza kupitia ukurasa wake wa Instagram kuwa akili ya Diamond ni kubwa sana toka mwaka 2009 hadi leo unazidi kupanda.
Wote Wanaotafuta, kujulikana, kutrend, kuongelewa lazima wakutumie wewe. Si madema, si wana?. Acha nitumie kauli hii wewe ni Bank ya Umaaruufu Tanzania (B.U.T)
Rayvanny anasema kila anayetafuta umaarufu au kuishika mitandao kijamii ni lazima amzungumzie Diamond. Twende pole pole, ndicho kilichonisukuma kuandika makala haya.
Kwa sasa kuna mabinti kadhaa wanajizolea umaarufu kwenye mitandao kwa kile wanachodai kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Diamond. Licha ya wengine kuongea wazi kabisa katika vyombo vya habari na wengine kwa kuficha muimbaji huyo yupo kimya kabisa kwenye hilo.
Hata hivyo dada wa Diamond, Esma Platnumz alishaonya kuhusu hilo. Esma alieleza kuwa hilo linajitokeza kwa sasa kutokana Diamond hajaweka wazi mahusiano yake au hajawa na mpenzi rasmi kama ilivyokuwa kwa Zari.
Hata hivyo kabla ya Diamond kuachana na Zari kulikuwepo na stori kama hizo lakini haikuwa kama sasa. Utakumbuka kuna kipindi video vixen Tunda alisemekana kuwa na ujauzito wa Diamond lakini wote walikanusha hilo.
Wakati Diamond akimtambulisha msanii Mbosso katika label yake ya WCB katika mahojiano na waandishi wa habari alieleza kushangazwa na hilo kwa kueleza yeye ni mwanume wa namna gani kila mwanamke mzuri anaambiwa ni wake.
Siku chache zilizopitia msanii Gigy Money katika mahojiano na Dizzim TV alidai kuwa baba wa mwanae ni Diamond. Ingawa inaonekana kauli hiyo alitoa kwa utani ila inasadifu kile nilichotangulia kueleza na kinachoendelea kwa upande wa Diamond.
Kwa sasa video Irene ambaye ameonekana katika video mbili za Rayvanny anagonga vichwa vya habari vilivyo kwa kile anachodai kuwa yeye ndiye amechukua nafasi ya Zari kwa Diamond. Twendele pole kwenye hili.
Ni drama juu ya drama kwa upande wa Diamond na zinakuwa nyingi kila kukicha kutokana muhusika mwenye amekaa kimya akitazama sinema ambayo mwenye ni muhusika. Je, haya unamjenga Diamond au yanambomoa kimuziki?.
Tunafahamu kuzungumziwa (publicity) ni sehemu ya mtaji mkubwa wa msanii na sanaa yake kwa ujumla. Huenda Diamond ananufaika nalo kwa upande wake mmoja au mwingine lakini inamtengenezea picha gani kwa wale wasiovutia na mambo hayo zaidi ya muziki wake.
Je, kuendelea kwa mambo kama hayo bado Waziri Mwakyembe atakuwa na mpango wa kumpa Diamond ubalozi wa maadili?, hakutaathiri muziki wake ashindwe kumkosha Mzee Augustino Mrema na wenzake?. Nawasilisha.