Mama asimulia mwanawe, mkwewe walivyofariki kwa kujichoma moto


MAMA wa Zainabu Juma aliyefariki dunia pamoja na mumewe Hussein Zaidi, amesimulia kilichotokea wakati wanandoa hao walipopoteza maisha baada ya mwanamume kuchoma moto chumba kisa wivu wa mapenzi.

marehemu Hussein Zaidi, akiwa na mke wake zainabu juma ambaye nae pia ni marehemu.

Zainabu (42) na Zaidi (58), waliofariki dunia kwa moto wakiwa chumbani kutokana na wivu wa mapenzi, walizikwa jana Kibaha mjini katika makaburi tofauti.

Wanandoa hao waliokuwa wakifanya biashara katika soko la Loliondo lililoko Halmashauri ya Mji wa Kibaha, waliteketea kwa moto baada ya mume kuwasha kwa makusudi moto ndani ya chumba walichokuwa wamelala baada ya kumtuhumu mke wake kuwa, alikuwa na mwanamume mwingine.

"Nakumbuka siku ya tukio saa saba hivi nilisikia kelele za kuomba msaada kutoka chumba cha mwanangu aliyekuwa amelala na mume wake. Alipiga yowe mamaaaaa, mamaaaa nioke ananiua, ananichoma kisu, mara ananiunguza.

“Nilijitahidi huku na kule kufungua mlango nikashindwa, ikabidi nipige kelele majirani watusaidie kwani milango yote ilikuwa imefungwa hatukuwa na pa kutokea na tulianza kuona moshi mkubwa ukitoka chumbani kwao,” alisema Bitiali Msangi, mama wa Zainabu.

Akizungumza kwa uchungu, alisema katika kipindi cha mwezi mmoja amepoteza watoto wawili. Alisema msiba huo umemkuta muda mfupi baada ya kutoka kijijini kwao mkoani Kilimanjaro kwenda mkoani Pwani kwa ajili ya msiba wa mtoto wake wa kiume, aliyefariki dunia.

"Nilikuja hapa mwezi mmoja uliopita baada ya mwanangu wa kiume kufariki dunia huko Chalinze. Baada ya maziko nikaja hapa kwa binti yangu kusubiri arobaini, ili tumalize msiba nirudi Moshi na arobaini ilitakiwa tufanye leo (jana). Mipango yote tumekamilisha na huyu Zainabu mwanangu ambaye naye amefariki dunia. Kwa kweli siamini hata kidogo,” alinyamaza kidogo na kuanza kulia kwa uchungu.

Akizungumza kwa masikitiko, mke mkubwa wa marehemu Zaidi, Evelina Sospeter (48), alisema alifunga ndoa ya Kiislamu na Zaidi mwaka 1988 na kubahatika kuzaa naye watoto wanne. Hata hivyo, alishindwa kuzungumza zaidi baada ya kuwa na uchungu wa kufiwa.

Habari kutoka kwa baadhi ya majirani zinasema mke mkubwa anayeishi eneo la Mwanalugali, alichukuwa jukumu la kuhamishia msiba nyumbani kwake na akamzika mumewe makaburi ya Mwanalugali huku Zainabu akizikwa na ndugu zake katika makaburi ya Loliondo.

KAMANDA ALONGA

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Blasius Chatanda, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa saba usiku huko Kilimahewa, Mailimoja Kibaha mkoani Pwani.

Akisimulia tukio lilivyotokea, Chatanda alisema awali mwanamume huyo alijaribu kumchoma mkewe kisu, lakini hakufanikiwa baada ya mke wake kukwepa ndipo alipoamua kukusanya nguo zao chumbani na kuziwasha moto ili azma yake itimie ya kutaka wote wafe.

Alisema baada ya mwanamume huyo kuwasha moto huo kwa kiberiti, walianza kuungua na ndipo mkewe alipiga kelele za kuomba msaada hadi majirani na polisi walipovunja mlango na kuwaokoa, lakini walikuwa wamekwishaungua mwili mzima.

Alisema walipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini baada ya muda mfupi walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Diwani wa Tangini, Theodory Joseph,  alisema wamepoteza mtu muhimu kwa kuwa Zainabu alikuwa mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kilimahewa kwa tiketi ya Chadema na Mwenyekti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kata ya Tangini.

"Tumepoteza mtu muhimu sana, alikuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya kata. Alikuwa mwanamke shupavu mchapakazi na jasiri asiyekubali kushindwa. Sisi wananchi wa Kata ya Tangini tutamkumbuka na kumuenzi kwa mazuri yote aliyofanya wakati wakati wa uhai wake,” alisema.

Joseph alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi hasa wanandoa kuepuka kuchukua uamuzi mgumu ikiwamo kujitoa uhai pindi wanapokutana na changamoto mbalimbali katika ndoa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad