Manara: Matatizo ya Yanga yangekuwepo Simba tungekuwa tunapambana kutoshuka daraja


Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, anaamini kwamba matatizo ya kiuchumi wanayopitia timu ya Yanga hivi sasa, kama yangekuwepo Simba basi timu ya hiyo ingekuwa inapambana kutoshuka daraja katika ligi kuu. 

Manara amesema hayo leo Juni 5, 2018 nchini Kenya, wakati wa mazoezi ya timu ya Simba kujiandaa na mchezo wa nusu fainali wa mshindano ya Super Cup yanayofanyika nchini humo, na kuoneshwa kukerwa na mashabiki wa timu ya Simba ambao hawana imani na timu kutokana na baadhi ya wachezaji mahiri kutokuwepo pamoja na timu katika mashindano. 

“Tuendelee kuwaamini hawa wachezaji, wakati mwingine mashabiki wa Simba wanatofautiana na mashabiki wa Yanga, sisi watu wa Simba tunadhani kwamba tuna wachezaji maalumu, mimi kwangu Star ni Simba Sport Club, ninavyoamini mimi matatizo ya Yanga sasahivi tungekuwa nayo Simba, basi tungekuwa tunapigania kutoshuka daraja, mashabiki wangeanza kutulaumu viongozi”, amesema Manara. 

Manara ameonesha kukerwa na tabia ya mashabiki wa Simba, kutupa lawama kwa kocha mkuu wa timu hiyo Pierre Lechantre, amesema “kocha huyo anayepewa lawama ndiyo aliyetupa ubingwa, mimi sisemi kwamba ni kocha bora sana lakini haifai kumtolea maneno, mnaivunja moyo timu” 

Msemaji huyo wa Simba ameongeza kuwa licha ya timu ya Yanga kukumbwa na changamoto mbalimbali msimu huu, lakini wachezaji, mashabiki na viongozi wa klabu hiyo waliungana pamoja mpaka mwisho wa msimu bila kujali matokeo ya uwanjani. 

Timu ya Simba kwasasa ipo nchini Kenya ikiendelea na mshindano ya Super Cup baada ya kufanikiwa kutinga nusu fainali kwa ushindi wa mikwaju ya penati 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks kutoka Kenya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad