Licha ya kwamba amekuwa mkimya sana lakini viongozi wa Yanga waliompelekea Yusuf Manji, kilio cha wanachama amewpa jibu la kutia moyo.
Manji alijiuzulu Uenyekiti Yanga mwaka mmoja uliopita ambapo kwenye mkutano wa hivi karibuni wa wanachama waligomea uamuzi wake na kuomba viongozi wengine wamfikishie ujumbe huo.
Wanachama hao walienda mbali zaidi kwa kusisitiza kwamba wako tayari kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo na Manji aingie kama muwekezaji.
Mmoja wa viongozi wa Yanga aliiambia Spoti Xtra jana kwamba barua hiyo ilimfikia Manji na akawapokea vizuri na baada ya kuwasikiliza akawaambia amewaelewa atawajibu baada ya mfungo na sherehe za Eid el Fitr zilizomalizika jana Jumamosi.
Habari zinasema kwamba siku yoyote kuanzia kesho, Manji atatoa tamko rasmi la mustakabali wake ndani ya Yanga ingawa viongozi wanaamini kwamba atarudi kutokana na jinsi wanavyomshawishi.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba vigogo wa klabu hiyo wamekuwa wakimsihi Manji arudi kwa kutumia watu mbalimbali wenye nyadhifa serikalini na tayari wameanza kuona mwanga kwani amekuwa akiwajibu kwamba watulie kwanza aweke mambo yake sawa.
Yanga kwa sasa imekuwa chini ya kamati maalum iliyoko chini ya Mwenyekiti Abbas Tarimba ambaye ameanza mchakato wa usajili.
CHANZO: SPOTI XTRA