Ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ameandika waraka akiizungumzia Singida United na kutaja chanzo cha timu hiyo kukosa mataji katika msimu uliomalizika wa 2017/18 ni aliyekuwa kocha wake Hans Pluijm.
Msemaji huyo ameandika waraka uliionesha masikitiko yake kwa klabu ya singida united kwa kile alichodai ina pesa za kutosha hawana shida kama vilabu vingine lakini imekuwa na matokeo ya kawaida sana msimu huu.
“Sikutarajia kabisa kwamba, Singida United watasumbuliwa kiasi cha kufungwa na timu kama Lipuli, Prisons, wapapaswe na wapapasaji, na wengineo wenye usajili wa kawaida, ambao hawana hakika kesho kutakuchaje, jasho lao kufutwa mpaka wapige kelele kama vyula wakati wa mvua huku wamejificha matopeni,tafakarini, mpatengeneze mlipopaharibu ili msimu ujao hali yenu iendane na hadhi yenu”, ameandika Massau Bwire.
Bwire ameongeza kuwa “Kumaliza ligi nafasi ya tano, kupigwa 3-2 fainali FA na Mtibwa wakati Watanzania wengi waliwapa nafasi kubwa ya ushindi ni aibu, au Alizeti inawachanganya? Kama ndivyo badilisheni kilimo, limeni ufuta!”
Timu ya Singida United imetangaza kocha mpya atayekinoa kikosi hicho msimu ujao ambaye ni Hemed Morocco aliyechukua mikoba ya Hans Van Pluijm ambaye ametimkia Azam FC.