Kati ya mambo yaliyotawala Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ni matumizi ya video za VAR (Video Assistant Referee) ambazo kazi yake ni kumsaidia mwamuzi mambo yanayoleta utata.
Wapo walioipinga waziwazi kwamba haina maana sana kwa kuwa baadhi ya uamuzi wa waamuzi ulikuwa wa kutatanisha. Haukuwa na ukweli kwenye matumizi yake.
Labda tu haikutangazwa kwa kiasi kikubwa, lakini matumizi ya VAR yalianza kwenye michuano ya Kombe la FA England pamoja na ile ya Carabao Cup lakini pia kwenbye ligi za Bundesliga, Ujerumani na ile ya Italia ya Serie A.
VAR inamsaidia mwamuzi lakini ina raha na machungu yake. Mkipata VAR kwa ajili ya kuwasadia mtafurahi lakini upande wa pili, VAR inasononesha kwa kuwa tukio lililofanyika lilishapita dakika kadhaa kabla ya kurejewa.
Katika fainali za mwaka huu, VAR imetumika lakini kumekuwa na kelele nyingi lakini bado matumizi yake ni uamuzi wa mwamuzi kutaka msaada wa mashine hiyo au anaweza kushauriwa lakini bado uamuzi wa mwisho unabakia kuwa wa mwamuzi mwenyewe.
Bao la Diego Costa dhidi ya Ureno, penalti ya Ufaransa dhidi ya Australia pia penalti ya Sweden ilipocheza na Korea Kusini ilikuwa raha lakini mashabiki wakiguna kwenye mechi ya Brazil na Uswisi kwamba VAR ilipata kigugumizi.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka Brazil limetuma waraka Fifa kutaka maelezo kwanini VAR haikutumika kwenye mchezo wao na Uswisi.
CBF inaitaka Fifa kutoa maelezo kwa kuwa teknolojia ya VAR kazi yake ni kumsaidia mwamuzi kwa matukio tata, lakini haikuwa hivyo.
VAR inatumika kwa ajili ya kusaidia mwamuzi na itakuwa ya kudumu baada ya kupata mafanikio kwa kiasi kikubwa kwenye teknolojia ya goli. Bodi ya Fifa iliyokutana mapema Machi huu iliamua kuwa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zitatumia VAR.
VAR ni mfumo wa mawasiliano ambao hutumika kwa ajili ya uhakiki wa makosa ambayo hayakuonekana kwa urahisi na mwamuzi.
VAR itatumika pale kwenye kitendo cha kuotea chenye kuleta utata. Bao litakubaliwa ama kukataliwa baada ya kuangalia kwenye teknolojia hiyo. Hata hivyo, teknolojia hii haiangalii sana eneo la kuotea, ni mwamuzi mwenyewe.
Ndiyo hasa mlengo wa mpango huu. Timu inaweza kuzawadiwa penalti baada ya uthibitisho wa VAR nje ya uamuzi wa awali wa mwamuzi kutoiona faulo ya viashiria vya penalti.
KADI NYEKUNDU YA MOJA KWA MOJA
Mchezaji anaweza kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kutumia VAR. Teknolojia hii si kwa ajili ya kutoa kadi za njano.
Kama mwamuzi atatoa kadi nyekundu kwa mchezaji ambaye hakufanya kosa, kama ilivyokuwa kwa Kieran Gibbs na Alex Oxlade-Chamberlain wakati Arsenal ilipolala mabao 6-0 kwa Chelsea mwaka 2014, hapo VAR inaweza kutumika na uamuzi kubadilika.
VAR imezuiliwa kwenye maeneo mengine ili isiharibu ladha ya mchezo. Hata hivyo, Sheria mpya za Fifa zinampa nafasi mwamuzi kutoa uamuzi wakati mwingine nje ya utaratibu wa VAR hata kama itaonekana VAR imeonyesha kuna tatizo. Mwamuzi ataangalia teknolojia ya VAR utata utakapotokea ambao itakuwa uwanjani na atakaporidhika, anaweza kubadilisha uamuzi wake wa awali kwa kuonyesha ishara ya video na kutolea uamuzi tukio.
Hata hivyo, mwamuzi anatakiwa kuwa na msimamo wake badala ya kusubiri afanyiwe uamuzi na VAR.
Mwamuzi anatakiwa kuruhusu mchezo kuanza na kuusimamisha baada ya sekunde 70 kwa kuhakikisha mpira uko katikati ya uwanja na si eneo la timu moja.
Fifa iliamua kuanzisha utaratibu wa VAR lengo likiwa kuhakikisha uamuzi sahihi unatolewa hasa kwenye maeneo ya utata.
Wakati wa matumizi ya VAR changamoto zinaibuka. Baadhi ya mashabiki watakuwa wakishangaa kwa kuwa ni kitu kipya, wanaweza wakalaumu, hasa katika viwanja visivyokuwa na skrini kubwa. Fifa inataka skrini kubwa za uwanjani kutumika kuonyesha mashabiki usahihi wa uamuzi.
Pamoja na kuwepo na teknolojia mbalimbali za marudio ya mchezo, shutuma nyingi zimekuwa kwenye tukio la penalti. Uamuzi wa penalti wengi wanataka ubakie kwenye uamuzi wa mwamuzi kwa mtazamo wake.
Suala la kukatiza mchezo na kuamua kuja kupiga penalti, inaondoa ladha ya mchezo kwa kuwa penalti inatakiwa palepale baada ya tukio la kuchezewa rafu au kushika ndani ya 18.
Tukio la kutumia VAR, pia linaongeza muda kwamba matumizi ya VAR yanatumia dakika zisizopungua tano na ndiyo maana dakika tano huongezwa.
Hata utamu wa bao kuendelea na mwendelezo wa mchezo, ile ladha inaondoka kwa kuwa bao linatakiwa kufungwa si kwa kulipanga.
Pia inaelezwa waamuzi wengi hawana utaalamu na VAR.