Viongozi 9 wa CHADEMA, akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe kupitia wakili wao wamewasilisha maombi chini ya hati ya dharura ya kutaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu isitishe usikilizaji wa kesi yao ya kufanya maandamano.
Maombi hayo yanayotarajiwa kusikilizwa June 28, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri yamewasilishwa na wakili utetezi, Peter Kibatala.
Katika maombi hayo namba 15/2018 upande wa utetezi umedai kuwa wanaomba usikilizwaji wa kesi hiyo usitishwe hadi pale Mahakama Kuu itakapoyapitia maamuzi yote yaliyotolewa na Mahakama ya Kisutu kuhusu kesi hiyo.
Naye Wakili wa serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ameiambia mahakama kuwa wamepokea nakala ya maombi hayo, hivyo wanaomba kuwasilisha majibu yao ya hati kinzani kesho June 28, 2018.
Awali wakili Nchimbi alieeleza mahakama kuwa kesi hiyo imeitishwa ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali (Ph).
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri ameiahirisha kesi ya msingi hadi July 2,2018.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika.
Katibu wa chama hicho Dk. Vicenti Mashinji, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Tarime mjini Esther Matiko na mbunge wa bunda, Esther Bulaya.
Katika kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 Mbowe na wenzake hao wanaokabiliwa na mashtaka 13 ikiwamo ya kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa uasi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai.
Makosa hayo yanadaiwa kutendeka Februari 16,2018 katika maeneo ya viwanja vya buibui, Mwananyamala na barabara ya Kawawa kinondoni mkwajuni
Mbowe na Wenzake Wawasilisha Maombi Mahakamani Kusitisha Kesi Yao
June 27, 2018
Tags