Mbunge Bwege Kufanya Maandamano Julai 1 Kuishinikiza Serikali

Mbunge Bwege Kufanya Maandamano Julai 1 Kuishinikiza Serikali
Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF) Suleimani Bungara, maarufu kama Bwege amemtaka Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, awe sehemu ya maandamano ya wananchi wa mikoa Lindi na Mtwara ili kuishinikiza Serikali kurudisha pesa za wakulima wa zao la korosho.


Bungara amesema hayo leo Juni 20, 2018 Bungeni Jijini Dodoma, wakati wa kuchangia hoja mjadala wa mapendekezo ya Bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kuongeza kuwa mpaka kufikia Juni 30,2018 Serikali iwe imerudisha pesa za korosho kwa wakulima takribani shilingi bilioni 81, kinyume na hapo wananchi watalazimika kufanya maandamano Julai 1, 2018.

“Mpaka Juni 30, 2018, kama hela yetu haikurudi tunakuomba mheshimiwa Spika uje Mtwara kupokea maandamano ya wakulima wa korosho wa Mikoa ya kusini, kwasababu inaonekana serikali ya CCM sawa na patasi haifanyikazi mpaka igongwe” amesema Bungara.

Bungara ameongeza kuwa maandamano hayo hayataweza kuzuilika mpaka pale wakulima wa zao la korosho watakapo rudishiwa fedha zao na kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kujiuzulu kama atashindwa kurudisha pesa hizo.

Kwa upande mwingine mbunge huyo amesema ataunga mkono mapendekezo ya Bajeti hiyo endapo Serikali itaongeza fedha katika miradi ya maji, kilimo, mifugo, uvuvi na elimu kwasababu ni sekta ambazo zinawagusa wananchi wengi moja kwa moja na ndiyo wapiga kura.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad