Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu amesema ununuzi wa ndege za Bombardier uliofanywa na Serikali hauna tija kwa wananchi wa jimbo lake iwapo huduma za afya na barabara hazijaboreshwa.
Kadutu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 20, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2018/19 bungeni mjini Dodoma.
Amesema umebaki mwaka mmoja kabla ya nchi kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, hivyo ahadi zilizotolewa zinapaswa kutekelezwa.
“Serikali imejenga reli, inanunua ndege hebu twendeni kwa wananchi, ujue ukienda kule Ulyankulu ukauliza Bombardier hawakuelwi, barabara mbovu, afya mbovu hawakuelewi,” amesema Kadutu.
“Pelekeni fedha barabara ziboreshwe, Tarura (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini) wapewe fedha. Bajeti iliyobaki ni moja ya kujadili kwa utulivu kwani akili itakuwa majimboni tu, tusaidieni ili mwaka 2020 tupete,” amesema.
Akigusia ahadi za kampeni za uchaguzi, Kadutu amesema waliahidiwa jimbo la Ulyankulu litakuwa wilaya lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
“Hamtaki kutupa eneo lakini mnasema ahadi za Rais zitatekelezwa, sasa hii ni ahadi ya Rais, alisema akiingia siku tatu tu tunapata wilaya,” amesema.
“Sasa imebaki mwaka mmoja tu na nusu yako mengi, mmetuahidi lami tena kilomita tatu tu lakini tunaona mambo ambayo hayako katika ilani yanatekelezwa. Tukisema…,mimi watu wa Ulyankulu wamenituma.”
Mbunge huyo amesema anashangazwa na mawaziri kutotembelea jimboni kwake huku wakionekana kupishana katika majimbo mengine jambo linalokatisha tamaa wananchi.