Siku chache baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema ni mpenzi mkubwa wa nyimbo za msanii wa Bongo Fleva, Ally Kiba.
Akizungumza na MCL Digital katika mahojiano maalum, Dk Bashiru amesema hata dereva wake anafahamu kuwa anampenda msanii huyo na kwamba akiingia katika gari hupiga nyimbo za Ali Kiba hadi mwisho wa safari yake.
“Kwa upande wa wasanii, mimi napenda sana nyimbo za Ally Kiba, dereva wangu ameshajua nikiingia kwenye gari anapiga tu nyimbo zote zinafululiza mpaka nashuka,”amesema.
“Ila sijui kama Ali Kiba ni mwana CCM ama la. Sitajali kama ni mwana-CCM kwasababu nyimbo zake zinafanya kazi niliyoisema ya kujengea watanzania hari ya kujiamini.”
Amesema wasanii wamewapamba sana Watanzania kitaifa na hata kimataifa na kwamba hata nafasi ya waafrika katika tasnia hiyo iko juu jambo ambalo limeleta heshima.
“Mimi sijali mahadhi kama ni ya kigeni ama kikabila kama ni ya Kiswahili kama ni taarabu ili mradi una maudhui kuna ujumbe. Na ndani ya CCM sisi tunadhamini sana sanaa na tunakitengo maalum ambacho kipo chini ya uenezi kinaongozwa na Polepole (Katibu wa Itikadi na Uenezi Humprey Polepole) ,”amesema.
Amesema ndani ya chama wana kikundi cha TOT na Vijana Jazz ambavyo anataka viimarike na kufanya kazi ya kukitangaza chama kuhusu mazuri ya nchi.
Amesema bila ya kuwa na michezo, Taifa halitatambuliwa, umoja hautokuwepo na hata hatua za maendeleo hazitatambuliwa na mataifa mengine.
Amesema CCM wanamiliki viwanja lakini bado haviko katika hali nzuri na kwamba atajaribu kuwekeza na kuvifufua ili viwe na mchango katika jamii.